Ngoma hii ya Harmonize ina mambo mazito

MWISHONI mwa mwaka 2018, Diamond Platinumz alikuwa matatani baada ya wimbo wake wa Mwanza Nyegezi alioshirikiana na Rayvanny kupigwa marufuku na Basata kwa kukosa maadili katika maudhui yake.

Diamond Platinumz ambaye wakati huo alikuwa kwenye ziara zake za kimuziki za Wasafi Festival aliupiga wimbo huo alipokuwa ziarani Mwanza, na ‘so’ kuwa kubwa zaidi.

Basata wakajihisi kudharauliwa na kumshushia rungu kubwa kwa kumfungia kufanya matamasha ndani na nje ya nchi.

Wakati rungu hilo lilishuka, tayari alikuwa anajiandaa na mfululizo wa matamasha makubwa nchini Kenya.

Lakini baadaye busara zikatumika, matamasha ya Kenya yakafanyika...maisha yakaendelea.

Diamond mwenyewe aliandika waraka mrefu kwenye moja ya akaunti zake za mitandao ya kijamii kutetea wimbo kwa kusema jina la wimbo huo limetafsiriwa vibaya kwa sababu Nyegezi ni sehemu ya mkoa wa Mwanza hapa nchini.

Lakini Basata walisema hawakuufungia wimbo huo kwa sababu ya jina, bali maudhui yake kwa ujumla.

Sasa ukiangalia maudhui yake ndani hakukuwa na sarakasi nyingi zilizoachwa wazi, japo watu wazima wanaelewa yaliyomo.

Lakini ukiangalia kwa makini, wimbo huu ulikuwa unasaidia katika kujenga maadili kwa sababu ni wakati ule ambapo video chafu za mwanadada Amber Rutty ndo zilikuwa zimevuja.

Anaposema anaongopa michezo michafu, ni kama anasaidia kukemea tabia zile na kukumbusha kwamba serikali ipo na itakushughulikia ukifanya uchafu.

Bado hadi hapo alikumbusha wenye kuvaa nguo zisizo na staha ambavyo serikali inaweza kuwashukia.

Lakini bado hakueleweka, akashukiwa kama mwewe.

ONE NIGHT STAND

Hivi karibuni msanii mwingine wa kizazi kipya Harmonize kwa kushirikiana na kijana wake, Ibrah ametoa wimbo unaoitwa One night stand.

Tukianza na jina tu, wimbo huu unaonyesha kuwa kuna jambo zito ndani yake.

Yaani unakutana na mtu, mnamalizana...mchezo unaishia hapo. Maudhui yake ni sawa na Single girl/Single boy ya Lady Jaydee na Ali Kiba ya mwanzoni mwa miaka ya 2010.

Baby all I need mi siwezagi kuzunguka

One night, one night, one night stand

Yaani nipe nikupe kabla hakujapambazuka

One night, one night, one night stand

Anasisitiza kabisa kwa kuweka wazi kwamba yeye anachotaka usiku mmoja...yaani kila usiku mpya.

Siku hizi kupenda penda kumepitwa na muda

One night, one night, one night stand

Yaani akikupa kula akisusa mwingine atakuja

One night, one night, one night stand.

Katika kutaka kuhalalisha anavyohamasisha, hapa Harmonize anataka kuaminisha kwamba Upendo eros ni mambo ya kizamani.

Hapa anapingana hata na maandiko matakatifu.

Kwa mfano, Biblia takatifu inasisitiza kuwa na mahusiano halali na ya kudumu - yaani ndoa, badala ya ngono ya usiku mmoja (1 Wakorintho 7: 8-9).

Katika sunnah za Kiislamu, dini yake Harmonize, mwanazuoni Iman Al Bukhaariy anasema: “Enyi vijana! Mwenye uwezo wa kuisimamia ndoa na aoe kwani huko ni kuweza kuinamisha macho na kuweza kuzikinga tupu na kama hamna uwezo, basi ni juu yenu kufunga kwani huko ndiko kwenye kinga.”

Lakini Harmonize anataka kutuaminisha tofauti.

Unaweza ukasema hapo kidogo kuna fumbo, japo kama watu wazima tunajua nini anamaanisha.

Ni jukumu letu sisi kama jamii kusadia wanajamii wenzetu na taasisi zetu za umma kufanya kazi zake vizuri. Asanteni.