Aliyetwaa dhahabu akiwa peku riadha Taifa anena

Dar es Salaam. Mwanariadha Mbaraka James ambaye aliibuka bingwa wa mbio za mita 1500 akiwa hana kiatu mguu mmoja, ameeleza namna alivyopambana na kumuacha nyota wa timu ya Taifa ya mchezo huo, Gabriel Geay katika fainali za mashindano yaliyofungwa Jumapili iliyopita.

Mbaraka aliibuka kinara katika mbio hizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuwanyanyua mashabiki ambao walimshangilia na kumfanya Geay, mmoja wa nyota wa timu ya Taifa kutoamini matokeo hayo.

Mwanariadha huyo anayetokea Bumbuli mkoani Tanga aliibuka kinara akiwa hajavaa kiatu kwenye mguu wake wa kushoto. “Tukiwa tumekimbia hadi mita 300 kuna mwanariadha alinikanyaga mguu, kiatu kikavuka mguuni,” alisema.

Alisema aliona akiinama ili avae kiatu hicho angeachwa, hivyo akalazimika kukiacha na kuendelea na mbio huku akikimbia pekupeku mita 1200 zilizosalia.

Akizungumzia ushindani kati yake na Geay, Mbaraka alisema mwanzo kabla mbio kuanza alikuwa na hofu kutokana na wapinzani wake ambao wengi wana uzoefu na vimo vikubwa.

“Kocha (John Valangati aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Mkoa wa Tanga) aliniambia umeingia fainali unakwenda kuchuana na nyota wa kimataifa.

“Alinieleza kuwa mbio zitakapoanza lazima wao wataondoka spidi, hivyo nisiwafuate, nibaki kwenye kundi la pili, hadi mita 300 za mwisho ndipo nitoke.

“Tulipoanza mbio uoga uliniondoka baada ya kukimbia mita 200 za mwanzo. Hata hivyo nilifuata maelekezo ya kocha, Geay alikuwa mbele yangu katika mizunguko yote hadi mita 300 za mwisho alikuwa yuko umbali wa kama mita 15 zaidi.”

Mwanariadha huyo alisema alianza kukimbia kama alivyoelekezwa na kocha na alipofika kwenye mzunguko wa mwisho, umbali wa mita 100 kumaliza mbio ndipo aliongeza kasi na kumpita Geay ambaye alimaliza wa pili.

Akizungumzia ushindi huo, kocha wake alisema ni mwanzo mzuri kwa Mbaraka ambaye alianza kushiriki riadha kwenye Mashindano ya Shule za Sekondari (Umisseta) mwaka 2015 akiwa kidato cha kwanza.

“Alipata medali ya kwanza katika mashindano ya 2018 kwenye mbio za mita 3000 na 1500 kwenye Umisseta, alipohitimu sekondari niliendelea kuwa naye kijijini nikimnoa na mara mojamoja akishiriki mbio za marathoni kabla ya kuja kwenye mashindano ya Taifa mwaka huu.”

Alisema katika mashindano ya Taifa, Mbaraka alikimbia kwa maelekezo aliyompa kwani kama angeamua kushindana mwanzo mwisho na Geay pumzi zingekata.

“Nilimwambia asishindane naye, amuache aende ila yeye aongeze kasi katika mzunguko wa mwisho, ndicho alichofanya na Tanga tumechukua medali ya kwanza katika mbio hizo,” alisema.