Nyie eti uzi wa Yanga umeisha!

IJUMAA ya wiki iliyopita Yanga ilitambulisha jezi zao za msimu huu mpya 2020/21 na jana wakatangaza kwamba, mzigo wote umekata fasta tu.

Jezi hizo ziliuzwa kila jezi moja Sh 35,000 ukiwa ni mzigo wa awali ambazo zote zimeshambuliwa kama njugu kwa mujibu wa Mkurugenzi wa GSM, Hersi Said ambao ndio wasambazaji na wauzaji rasmi wa uzi huo.

“Tulileta jezi 8,000 tu na hizo zilikuja kwa ndege na leo (jana) zinakuja nyingine 8,000 tunawashukuru wanayanga kwa kununua bidhaa zao ila wasijali mzigo utakuja mwingi sana,” alidai Hersi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Usajili Yanga.

Alidai mzigo huo wa awali umeuzwa jijini Dar es Salaam pekee huku utakaoingia ndio utasambazwa katika maeneo mengine nchini.

Aliongeza kuwa walichelewa kutambulisha jezi hizo na kuzileta hapa nchini kutokana na changamoto ya corona.

“Tutakuwa nazo jezi zenye majina ya wachezaji wetu, tutazitengeneza kwa oda maalum kwa watu wetu mfano jezi ya Tonombe mtu anaweza kuhitaji idadi fulani tukamte ngenezea,” alisema Hersi.

Alisisitiza kuwa kwa sasa wameanza na jezi huko usoni watakuwa na vifaa mbalimbali vyenye nembo ya klabu hiyo ambazo wanayanga watapata fulsa ya kuziotumia.

ISHU YA KAPTENI

Katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga imeanza na manahodha wawili tofauti.

Katika mchezo wa kwanza dhidi Prisons Yanga ilimpa kitambaa Deus Kaseke, ambaye pia alikuwa kiongozi katika mchezo wa Wiki ya Mwananchi.

Juzi, Yanga ilipocheza dhidi ya Mbeya City mambo yakageuka na Haruna Niyonzima akavaa kitambaa cha nahodha huku Kaseke akianza kwenye mchezo huo.

Baadaye Niyonzima alipotoka kipindi cha pili kitambaa kikatua kwa beki aliyeipa Yanga ushindi Lamine Moro sasa hali hiyo imewafanya watu kuchanganyikiwa wasijue nani ni nahodha halisi.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amelieleza Mwanaspoti kuwa bado cheo hicho kilichoachwa wazi na aliyekuwa kiungo wao Papy Tshishimbi hakijapata mwenyewe rasmi.

Saleh, ambaye ni meneja mkongwe zaidi alisema kocha wa timu hiyo Zlatko Krmpotic hajafanya uamuzi wa nani awe nahodha wake.

“Kocha bado hajafanya uamuzi kwa sasa tunawapa nafasi kulingana na uzoefu kwa wale ambao, wanaanza uwanjani,” alisema na kuongeza:

“Kocha alitaka muda kwanza kuangalia nani atamfaa katika majukumu hayo, lakini siku si nyingi atafanya uamuzi wa kina nani watafaa katika majukumu ya kuwaongoza wengine uwanjani.”