UTAMU MTUPU : Van de Beek atakavyoleta mifumo kibao Man United

MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer kichwa kinampasuka kwa namna gani atamtumia kiungo mpya Donny van de Beek kwenye kikosi cha pamoja cha Bruno Fernandes na Paul Pogba.

Kocha huyo kwa sasa anahaha kukamilisha dili la Jadon Sancho na kwa hali ilivyo, dili hilo linaweza lisikamilike kwa wakati na Man United itarusha kete yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England Jumamosi dhidi ya Crystal Palace bila huduma ya Mwingereza huyo.

Ligi Kuu England imeshaanza, kwa timu kibao kucheza mechi zao – lakini kwa mashabiki wa Man United bado hawajaona kile ambacho timu yao itafanya kwa sababu mechi yao ya kwanza iliahirishwa kwa sababu walikuwa na majukumu kwenye Europa League hadi kwenye hatua za mbelembele, hivyo hawakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Na sasa watashuka uwanjani Jumamosi kukipiga na Crystal Palace, ukiwa ni mchezo wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu England.

Kocha Solskjaer amekuwa akipendelea kutumia fomesheni ya 4-3-3, lakini kama atatumia mtindo huo basi mchezaji mmoja hapo kati ya Pogba au Van de Beek anapaswa kuwa na nidhamu kubwa sana ya mchezo, kwa sababu atatakiwa kucheza kwenye kiungo ya kukaba.

Je, Solskjaer anatakiwa kufanyaje ili kumfanya Van de Beek kuingia moja kwa moja kwenye kikosi chake cha kwanza kwa kuwatumia sambamba na mastaa Pogba na Fernandes?

Haya hapa machaguo ya mtindo wa uchezeshaji ambao Solskjaer anaweza kuchagua ili kutoa nafasi kwa mastaa wake wote hao watatu kwenye safu ya kiungo kucheza kwa pamoja.

4-3-3

Hii ni fomesheni kipenzi kwa mashabiki wa soka kwa sababu inatoa fursa ya timu kuwa na wachezaji sita kwenye eneo la adui inapofanya mashambulizi. Lakini, kwa kuwatumia viungo hao wote watatu kwenye fomesheni hii, kutaifanya safu ya ulinzi kuwa na matatizo – la basi kati ya Pogba au Van de Beek mmoja anapaswa kuwa na nidhamu zaidi ya kukaba kuliko kwenda mbele kushambulia. Washambuliaji Mason Greenwood na Marcus Rashford watakuwa pembeni, watapaswa kuweka mkazo zaidi katika kurudi nyuma kuwasaidia mabeki wa pembeni kukaba timu itaposhambuliwa. Kwa mastaa waliopo, mfumo huu utawafanya Man United kuwa tishio sana inapokwenda mbele kushambulia kama itawatumia viungo wake wote watatu ambao ni balaa kwa kupiga pasi za mwisho na kutengeneza nafasi za kufunga.

4-2-3-1

Kwenye mtindo huu, Solskjaer anaweza kufanya uamuzi wa kuamua kuua winga moja - kwa kumtumia kiungo Pogba kwenye upande wa kushoto. Huu ni mfumo mzuri zaidi kwenye mechi ambazo timu pinzani zimekuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira muda mwingi. Solskjaer atakuwa amewatumia viungo wake wote watatu kwa pamoja, lakini shida ni kwamba hatakuwa na winga moja yenye kasi kubwa, kwa sababu Pogba atakuwa kushoto, huku kulia kunaweza kuwa na ama Greenwood au Rashford wakishambulia kutokea kwenye eneo hilo. Kwa mastaa hao kucheza pamoja, Man United itakuwa na nguvu kubwa sana kwenye sehemu ya kiungo, huku Nemanja Matic akiwajibika kwa jambo moja tu, kukaba ilhali shughuli ya kushambulia na kutengeneza nafasi za kufunga itafanywa na Van de Beek, Pogba na Fernandes.

4-5-1

Fomesheni hii ya 4-5-1 inaweza kubadilika muda wowote na kuwa 4-3-3. Kwa msimu uliopita, Solskjaer aliijaribu mara kadhaa, lakini haikumletea matunda makubwa sana ndani ya uwanja. Kwa ujio wa Van de Beek kwenye kiungo ya Man United kunaweza kuifanya timu hiyo kuwa na nguvu kubwa na kutumia mfumo huo wa 4-5-1 bila ya matatizo, kwa sababu itakuwa na wachezaji wengi kwenye eneo la katikati ya uwanja wenye uwezo wa kufunga.

Matakwa ya mfumo huu wa kiuchezaji unahitaji wachezaji wenye kasi kubwa pembeni na hapo, mastaa kama Rashford na Greenwood watacheza kwenye nafasi hizo, huku Martial akikabidhiwa majukumu kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati ili kuwa na kazi moja tu, kutupia mipira nyavuni.

3-5-2

Hii ni fomesheni ambayo Solskjaer aliitumia sana msimu uliopita na kumpatia mafanikio makubwa.

Mabeki wa kati watatumika, ambapo Luke Shaw atakuwa beki wa tatu wa kati akicheza sambamba na Harry Maguire.

Kwenye mtindo huo, mabeki wa pembeni, Brandon Williams na Aaron Wan-Bissaka watasogea mbele kidogo kuunda kundi la wachezaji watano watakaokuwa kwenye mstari wa kati, ambapo viungo Matic, Fernandes na Pogba watahusika. Lakini, kwenye mfumo huu, Solskjaer atakuwa na jambo moja, kuamua ni mchezaji yupi wa kumwaanzisha kati ya Pogba na Van de Beek. Ni mfumo ambao bila ya shaka, Solskjaer anaweza kuutumia kwenye mechi ngumu kama za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

3-4-3

Solskjaer haonekani kabisa kama anaweza kuitumikia fomesheni hii, ambayo imelenga zaidi kwenye kushambulia. Mfumo huu utampa nafasi ya kutosha ya kuwatumia wachezaji wake sita matata kabisa kwenye safu ya ushambuliaji.

Washambuliaji watatu Martial, Rashford na Greenwood wote watakuwapo ndani ya uwanja kwenye safu ya ushambuliaji, huku viungo wote watatu matata, Pogba, Fernandes na Van de Beek huku Matic akiwa na kazi moja ya kuwalinda mabeki wa kati, ambao ni Luke Shaw, Maguire na Victor Lindelof.

Solskjaer atatumia mtindo huu wa kiuchezaji kwenye mechi ambazo atahitaji kushambulia mwanzo mwisho huku akicheza dhidi ya wapinzani ambao si tishio sana kwa maana ya kutoa adhabu kwa timu yake.