Wasauzi wawili watimka Yanga

Muktasari:

Kikosi cha Yanga leo Septemba 16, 2020 kitacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi

MAKOCHA wawili wa Yanga raia wa Afrika Kusini wametoweka ghafla kwenye benchi la timu hiyo huku kukiwa na taarifa wameenda kwao.

Wasauzi hao ni Reidoh Berdien ambaye ni kocha msaidizi wa tatu akiwa na utaalamu wa mazoezi ya viungo, pia daktari wa viungo, Farid Caseem.

Katika mechi dhidi ya Mbeya City hawakuonekana kwenye benchi badala yake alikuwepo Kocha Mkuu Zlatko Krmpotic na msaidizi wake wa kuwanoa makipa Vladimir Niyonkuru raia wa Burundi.

Kukosekana kwa makocha hao wawili kumeibua sintofahamu kwenye mitandao ya kijamii lakini uongozi umefafanua wameondoka nchini lakini kwa ruhusa maalumu.

Msemaji wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema wawili hao wamerudi kwao Afrika Kusini kwa mapumziko ya muda mfupi kwa kuwa makocha hao hawakupata muda wa kupumzika ligi ilipomalizika hasa baada ya Luc Eymael kupigwa chini.

Amesema wawili hao watarejea nchini baada ya wiki moja kuja kuendelea na majukumu yao.

Bardien na Caseem walikuja nchini kwa kuletwa na aliyekuwa kocha wa Yanga Luc Eymael ambaye baadaye alitimuliwa lakini Yanga alithibitisha wawili hao wataendelea kubaki katika ajira zao.