Wema chunga sana

Muktasari:

Wataalam wafichua athari za kujipunguza kupita kiasi

USIBISHE, mwanadada Wema Sepetu hajawahi kutoka midomoni mwa watu tangu amekuwa staa nchini. Ndio, tangu alipowagaragaraza warembo wenzake kwenye Miss Tanzania wilaya, mkoa hadi Taifa mwaka 2006 amekuwa gumzo kwa kila anachokifanya.

Kazungumzwa alipojitosa Bongo Movie, akajadiliwa sana alipokuwa na mahusiano na Steven Kanumba mpaka Diamond Platnumz. Yaani kitu chochote anachofanya hakiachwi na bahati nzuri ni mwenye nyota ya kupendwa na mashabiki.

Achana na stori zote za nyuma kuhusiana na mambo ya malavidavi mpaka kuingia Chadema na kutoka, kwa sasa amekuwa gumzo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ishu ya kujipunguza ghafla mwili na kuwa kimbaumbau.

Iko hivi, aliposhinda Miss Tanzania, Wema alikuwa mwembamba kama ambavyo mamiss wengi huwa, kisha akajiachia na umbile lililowachanganya watu. Kila mdada alitamani awe na shepu kama yake, lakini katikati ya 2018, mkali huyo wa filamu alipotea kwa muda kabla ya kurejea mwishoni mwa mwaka huo akiwa na muonekano tofauti akipungua kutoka ubonge hadi kipotabo. Karibu kila shabiki mtandaoni alikuwa na lake kuanzia njia ambazo Wema alizitumia kupunguza mwili mpaka jinsi anavyoonekana baada ya kupunguza mwili.

Wapo waliosema eti alikata utumbo, ingawa mwenyewe alikanusha na kusema njia aliyoitumia ni kula vyakula maalumu, kufanya mazoezi na kunywa dawa mbalimbali. Huku baadhi ya mashabiki wakidai kupungua kwake hakujampendezesha jambo ambalo anasema hajali kwani hata alivyokuwa mnene kuna waliosema hapendezi na kufikia hatua ya kumpa majina mabaya.

MAMBO YAANZA UPYA

Lakini watu wakiwa wameanza kusahau kumfuatilia juu ya ukimbaumbau wake, ghafla akabadili upepo na gumzo baada ya picha inayomuonesha akiwa kwenye mkutano wa CCM.

Wazomeaji wa mitandaoni wakaichukua picha hiyo na kuifananisha na ya mtu aliyeigiza kwenye filamu ya maisha ya Yesu, yaani yule aliyetolewa mapepo kwake na kupelekwa kwa nguruwe.

Hata hivyo, wasichokijua wengi ni kwamba Wema sio msanii wa kwanza kupunguza mwili duniani, kwa mfano hapa Tanzania mbunifu wa mavazi Mustafa Hassanali alishawahi kupunguza na huko majuu msanii kama Adele na Rick Ross pia walijipunguza.

Inaelezwa Rick Ross alipunguza kilo 45 baada ya kushauriwa na madaktari kupungua kwa sababu alikuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa yanayohusiana na unene.

Mbali ya masuala ya afya, pia mambo yake ya kuigiza na mitindo zimekuwa sababu ya Wema kupungua ambapo anaeleza kuwa wakati alipokuwa bonge kulikuwa na baadhi ya nafasi hawezi kuigiza kwa sababu zilikuwa haziendani na mwili wake.

“Nilikuwa nakosa kazi nyingi kwa sababu nilikuwa mnene na nilikuwa siendani na hizo roles. Hiyo ni sababu nyingine kutaka kupungua,” alieleza Wema. Mbali na uigizaji, kazi nyingine anazofanya Wema zinahusiana na mambo ya urembo, sekta ambayo kipindi hiki inahitaji wanawake wembamba na warefu, kwa hiyo huko alikuwa anakosa madili.

MwONEKANO TATIZO

Jingine ni mwonekano. Kwa kawaida kila mtu anatafsiri ya muonekano mzuri, lakini katika nyakati hiz watu wengi hasa wanawake wamekuwa wakiamini mwanamke mwembamba ana mwonekano mzuri zaidi.

Adele alipungua kwa sababu za kimuonekano wakati Wema amewahi kukakiriwa akisema anajiona anapendeza kuwa na mwili mdogomdogo. “Kuwa mdogomdogo raha sana, ukiwa mnene kuna baadhi ya nguo inabidi zikupite, lakini sasa hivi naweza kuvaa nguo staili yoyote. Nainjoi na haka kamwili jamani,” aliandika hivyo kwenye Instagram yake.

WASIKIE WATAALAMU

Kutokana na kuwa gumzo kwa mwonekano wa mrembo huyo kila anapopita, Mwanaspoti liliwatafuta wataalamu waliozungumzia athari na nini Wema anapaswa kufanya.

Dk Colman Living, daktari wa magonjwa ya kinamama wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema hakuna ugonjwa wa kizazi unaotokana na kuzungukwa na mafuta kama anavyosema Wema.

Anasema kuna hali zinatokea kwenye mwili wa mwanamke ambazo husababisha tatizo la kutoshika mimba.

Mojawapo, anasema ni pamoja na unene uliopitiliza kwa sababu kuna homoni zinazolishwa mwilini na kusababisha mayai kushindwa kupevuka. “Mtu anapofikia hatua hii ndio hapo anashauriwa kupungua kidogo na sio sana kama alivyopungua Wema,” anasema.

“Dalili ambazo mtu ataziona kwa kuwa na unene uliopitiliza ni pamoja na kubadilika mara kwa mara kupata siku zake za hedhi. Mfano badala ya kuona siku 28 unaweza kwenda mpaka siku 35 au kupungua zaidi.

“Pia ukipima uzito wako na urefu wako (BMI) utaona haviendani na hapo ndipo unaweza kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na ugonjwa wa moyo.”

Hata hivyo, mtu ambaye ana tatizo hilo, daktari huyo anasema kuna dawa hupewa kushtua homoni ambazo zinasababisha mayai kutopevuka.

Athari anazoweza kuzipata, Dk Colman anasema mwanamke akinenepa sana ni tatizo hivyo kinachotakiwa ni kufuata ushauri wa madaktari ambao wataangalia urefu na uzito wa mhusika na kumwelekeza cha kufanya.

KIPI KINAZUIA MIMBA

Cha kwanza ambacho kinaweza kumfanya mwanamke asishike mimba, Dk Coman anasema ni kuziba kwa mirija ya uzazi kwa kuwa hii ndio kila kitu katika kupitisha mbegu za kiume.

Hivyo mwanamke akiwa na tatizo hili hupimwa kwa kutumia dawa maalumu ambayo hupitishwa kupitia uke au kwa njia ya matundu (laparascopy),” anasema

Yai lililotunga mimba kule lilipotoka kunatakiwa kuzalishwa homoni za ‘prosetojeni’ lakini wenye tatizo la unene uliopitliza baadhi hujikuta wakipoteza uwezo huo na hivyo mimba ikifika mahali fulani inaharibika na kutoka. “Homoni hizo hupitishwa katika mfumo wa damu, ambapo yai lililoingia likitoka kuna kovu huacha na huo ndio uhai wenyewe wa mimba ambao unatakiwa kupaliliwa na hizo homoni, hivyo kama mtu hana uwezo wa kuzizalisha ni wazi mimba haiwezi kukua.”

NINI KIFANYIKE?

Mtu anayepitia matatizo ya aina hiyo anapaswa kufanya kama anataka kushika mimba au atashika mimba ni pamoja na kutokuwa na mawazo ya kimwili au kiakili’ na kupata muda mwingi wa kupumzika. Jingine ni kutumia dawa zinazoitwa folic acid zinazosaidia mjamzito katika ukuaji wa mtoto tumboni ikiwemo kumuepusha na ugonjwa wa mgongo wazi na vichwa vikubwa anapozaliwa.

LISHE YAKE JE?

Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi, kutoka taasisi ya Chakula na Lishe, Adeline Munuo anasema upunguaji wa kilo kwa kasi kwa mrembo huyo ni hatari kwa afya yake.

Anasema iwapo Wema atanenepa anaweza kupata tatizo la mifupa kukosa nguvu, suala ambalo ni baya.

Athari nyingine ni kushuka kwa kinga za mwili hivyo anapopatwa na ugonjwa inakuwa vigumu kukabiliana nao.