Sauti za Busara kumenoga, wasanii kila kona

Muktasari:
Tamasha la 17 la Sauti za Busara limezinduliwa rasmi leo Februari 13 visiwani Zanzibar huku wakiwaenzi wa moja wa waasisi wa tamasha hilo ambao ni Ruge Mutahaba na Makame Faki Makame ambao ni marehemu kwa sasa
SAUTI za Busara moja ya Tamasha kubwa barani Afrika limezinduliwa jana Ijumaa eneo la kihistoria la Ngome Kongwe likiwa na orodha kubwa ya wasanii kutoka kila kona.
Akizungumza na Waandishi wa Habari visiwani Zanzibar hapa, Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud aliwasihi Watanzania na wageni ambao wamefika kutoka kila kona ya ulimwengu kujumuika kwa pamoja na kushuhudia kwa kushiriki tukio hilo la aina yake.
“Tunaanza tamasha hili la aina yake katika mwaka, wakati Zanzibar itakuwa inaandaa siku nne mchana na usiku bila kusimama kwa muziki wa kiafrika chini ya anga la Afrika, tamasha lina majukwaa matatu ambayo yote kwa asilimia 100 wanamuziki watapiga muziki ‘live’ ikiwamo muziki utakaokuwa unapigwa bure kwenye bustani za Forodhani” alisema Mahmoud
Mwenyekiti wa bodi ya Busara promotion Mohamed Simai , ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amesema ni furaha kuona wazo la watu saba leo limekuwa wazo la watu wengi ambao wanapata faida nalo.
"Tulianzisha tamasha hili watu saba leo hii limekua na mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi, jamii inafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na tamasha hilo" alisema Sumai.
Aliongeza kuwa katika timu ya watu saba waasisi wa tamasha hilo alikuwepo Marehemu Ruge Mutahaba pamoja na Mzee Makame Faki Makame ambapo hili ni tamasha la 17 la Sauti za Busara.