Makocha hawa mashabiki wanatamani kuwaona Kombe la Dunia

Muktasari:
- Kuna mambo kibao yanayotofautisha soka la klabu na timu ya taifa baada ya kushuhudia makocha kibao waliokuwa mahiri wakati wanazinoa klabu, lakini mambo yalikuwa ovyo kwenye timu za taifa.
LONDON, ENGLAND: FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zimebakiza mwaka mmoja tu kuanza, huku mashabiki wengi wakitamani kuona baadhi ya makocha wa kwenye timu za klabu wapewe dili za timu za taifa ili wakaonyeshane ubabe katika michuano hiyo.
Kuna mambo kibao yanayotofautisha soka la klabu na timu ya taifa baada ya kushuhudia makocha kibao waliokuwa mahiri wakati wanazinoa klabu, lakini mambo yalikuwa ovyo kwenye timu za taifa.
Kutokana na hilo, kuna makocha saba ambao mashabiki wangependa kuwaona wakichuana kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 ili kuona nani mbabe wao wanapohamia kwenye soka la kimataifa.

Carlo Ancelotti
Akiwa ameshinda kila kitu kwenye ngazi ya klabu, Mtaliano Ancelotti bila shaka atakuwa na hamu kubwa ya kwenda kufanya jambo la maana kwenye soka la kimataifa akiwa na timu za taifa. Hivi karibuni iliripotiwa ataachana na Real Madrid na kinachoripotiwa atakwenda kufanya kazi kwenye timu ya taifa. Kazi yake ya ukocha alianza kama msaidizi wa Arrigo Sacchi kwenye timu ya taifa ya Italia, hivyo ameshaonja utamu wa soka la kimataifa. Ancelotti kwa sasa anahusishwa sana na timu ya taifa ya Brazil na kama atakamatia kibarua hicho, bila ya shaka atakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.

Jose Mourinho
Mourinho ni kocha mwingine anayesubiriwa kwa hamu kuona atakwenda kufanya nini atakapokabidhiwa mikoba ya kuinoa timu ya taifa baada ya kupata mafanikio makubwa kwenye ngazi ya klabu. Hata ndoto za kocha huyo Mreno siku moja kwenda kuinoa timu katika fainali za Kombe la Dunia. Kwa sasa ni kocha wa klabu ya Fenerbahce, lakini Mourinho aliyetambulisha mwenyewe kama Special One anaweza kushawishika na kibarua cha kwenda kuinoa timu ya taifa hasa kwenye fainali kubwa ikiwamo za Kombe la Dunia 2026. Mourinho mwenyewe aliwahi kusema kuhusu mipango ya baadaye akitaka kushiriki kwenye michuano tofauti kama Kombe la Dunia au michuano ya Euro.

Pep Guardiola
Kutokana na kocha Mhispaniola, Pep Guardiola kuwa na mkataba kwenye kikosi cha Manchester City hadi 2027, hivyo haionekani kama kutakuwa na uwezekano wa kuinoa timu ya taifa kwa mwaka 2026, lakini kwenye soka chochote kinaweza kutokea muda wowote. Guardiola aliwahi kuulizwa kuhusu mipango yake ya baadaye na alifichua kilichopo mbele yake ni kufanya kazi kwenye timu ya taifa, angependa kuandaa timu yake kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia au michuano ya Euro. Kuna kipindi Guardiola alihusishwa sana na timu za taifa za Brazil na England, lakini anaweza kukubali mikoba pia ya kwenda kuinoa timu ya taifa ya kwao, Hispania.

Gennaro Gattuso
Soka la kimataifa lina mambo yake na moja ya watu wanaotazamwa wanaweza kwenda kufanya vizuri kwenye timu za taifa watakapoamua kufanya hivyo ni Kocha Gennaro Gattuso. Tangu alipoanza kazi yake ya ukocha mwaka 2013, Gattuso tayari ameshazionoa klabu tisa tofauti na katika kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026, kocha huyo atakuwa na uzoefu wa kutosha wa kupewa moja ya timu ili kwenda kuonyesha ubabe wake. Baada ya kuwamo kwenye sehemu ya kikosi cha Italia kilichonyakua ubingwa wa Kombe la Dunia 2006, Gattuso anafahamu kitu gani cha kufanya ili kunyakua mataji yenye hadhi kubwa kama hayo kwenye mchezo wa soka.

Diego Simeone
Si kitu unachokitazamia kutokea sasa hivi kumwona kocha Diego Simeone akiondoka Atletico Madrid, lakini kama atafanya hivyo basi bila ya shaka safari yake itakuwa kuelekea kwenye majukumu ya kuwa kocha wa timu ya taifa. Kocha huyo aliyekuwa kiungo matata kabisa wa timu ya taifa ya Argentina wakati anacheza soka, bila ya shaka atakuwa mwenye matamanio makubwa ya kwenda kuinoa timu hiyo ya taifa kwenye michuano mingine kama Kombe la Dunia. Wakati mwaka mmoja umebaki kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026 kuanza huko Marekani, mashabiki wangetamani kuona fainali hizo pia zinashirikisha makocha mahiri na mashuhuri kwenye soka la dunia.

Antonio Conte
Kocha Antonio Conte aliwahi kuinoa timu ya taifa ya Italia kwa miaka miwili, lakini kwa muda wake huo hakupata fursa ya kukiongoza kikosi cha Azzurri kwenye michuano mikubwa kama ya fainali za Kombe la Dunia. Jambo hilo limewanyima mashabiki wa soka kumshuhudia kocha huyo mwenye mbinu nyingi kuona ni kitu gani angeweza kukifanya kwenye fainali kubwa kama hicho. Kwa sasa ameelekeza nguvu zake katika kuhakikisha anaifanya Napoli inafanya vizuri kwenye michuano mbalimbali ikiwamo ya Serie A, lakini matumaini ni makubwa kwa kocha huyo kurudi kwenye michuano ya soka la kimataifa na kuwa na moja ya timu ya taifa kwenye fainali kubwa, hasa za Kombe la Dunia.

Jurgen Klopp
Aliachana na Liverpool mwaka jana na sasa kocha Mjerumani, Jurgen Klopp amekwenda likizo ya ukocha, akipata kazi ya kuwa bosi mkubwa kwenye klabu za Red Bulls, RB Leipzig na RB Salzburg. Siku za karibuni jina lake lilihusishwa na klabu ya Real Madrid, lakini kinachoonekana ni Xabi Alonso ndiye atakayekwenda kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Bernabeu kuchukua nafasi ya Kocha Carlo Ancelotti, atakapoondoka mwishoni mwa msimu. Lakini, kwa Klopp kuendelea kuwapo tu na kutokuwa na kazi ya ukocha kwa sasa hilo linaweza kuzivutia timu za taifa zikaamua kumpa kazi mapema kwa ajili ya kwenda kuwaongoza kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.