Atletico yajitosa kwa Antony, Juventus, Villarreal zatajwa

Muktasari:
- Staa huyu ambaye msimu huu ameonyesha kiwango bora akiwa kwa mkopo Real Betis, mkataba wake wa sasa na Man Uniter unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
ATLETICO Madrid imepanga kufanya mazungumzo na wawakilishi wa winga wa Manchester United, Antony, 25, ili kumsajil katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Staa huyu ambaye msimu huu ameonyesha kiwango bora akiwa kwa mkopo Real Betis, mkataba wake wa sasa na Man Uniter unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Mbali ya Atletico huduma ya Antony ambaye msimu huu akiwa na Man United na Betis amecheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao tisa, pia anawindwa na Juventus na Villarreal.
Mbali na uwezo mkubwa wa kufunga aliouonyesha akiwa na Betis tangu Januari staa huyu pia ametoa asisti tano.
Mabosi wa Betis pia wanapambana sana ili mshambuliaji huyu abaki lakini changamoto kubwa inaonekana kwenye pesa anazohitaji kama mshahara ambazo kwao ni kubwa.
Tijjani Reijnders
MANCHESTER City inataka kumsajili kiungo wa AC Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Tijjani Reijnders dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Vigogo wa Milan wapo tayari kumuuza fundi huyu lakini hawatosikiliza ofa yoyote itakayokuwa chini ya Pauni 57 milioni. Tijjani ni mmoja kati ya mastaa ambao wanahusudiwa sana na Kocha wa Man City, Pep Guardiola na huenda akatua kikosini hapo mwisho wa msimu kwani kocha huyo anataka kuwa na kikosi imara msimu ujao.
Jeremie Frimpong
LIVERPOOL inapambana kuipata saini ya beki wa kulia wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Uholanzi, Jeremie Frimpong katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ajili ya kuziba pengo litakaloachwa wazi na Trent Alexander-Arnold anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu kutua Real Madrid. Ripoti zinaeleza Leverkusen ipo tayari kumwachia fundi huyu lakini kama timu inayomhitaji italipa kiasi kisichopungua Pauni 33 milioni.
Sven Botman
BEKI kisiki wa Newcastle, Sven Botman anataka kuendelea kusalia katika kikosi hicho licha ya kupata ofa kutoka Paris St-Germain inayohitaji kumsajili mara baada ya msimu huu kumalizika. Staa huyu wa kimataifa wa Uholanzi kwa sasa ana umri wa miaka 25, na amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Newcastle tangu kuanza kwa msimu huu.
Kevin de Bruyne
Napoli bado inafanya mazungumzo na kiungo wa Manchester City na Ubelgiji, Kevin de Bruyne kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Hivi karibuni ilithibitishwa kiungo huyu ataachana na Man City ifikapo mwisho wa msimu huu. Mbali ya Napoli anahusishwa na baadhi ya timu za Marekani na Saudi Arabia.
Theo Hernandez
REAL Madrid inataka kumsajili beki wa kushoto wa AC Milan na timu ya taifa ya Ufaransa, Theo Hernandez katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Beki huyu kisiki ambaye ni tegemeo kwa sasa katika kikosi cha kwanza cha Milan awali aliwahi kuitumikia Real Madrid miaka sita iliyopita kabla ya kuachana nao na kutua Milan.
Evan Ndicka
ARSENAL huenda ikakutana na upinzani mkali kutoka kwa Paris St-Germain kwenye harakati zao za kuiwania saini ya beki kisiki wa AS Roma sign Roma na timu ya taifa ya Ivory Coast, Evan Ndicka kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Roma ipo tayari kumuuza fundi huyu lakini kwa kiasi cha pesa ambacho hakitopungua Pauni 25 milioni.
Enzo Fernandez
CHELSEA haina mpango wa kumuuza kiungo wao raia wa Argentina, Enzo Fernandez dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya tetesi zinazodai fundi huyu anaweza kujiunga na Real Madrid iliyoanza kuinyatia huduma yake tangu dirisha la majira ya baridi mwaka huu. Enzo ambaye alisajiliwa kwa dau nono la Pauni 107, kwa sasa ana umri wa miaka 24.