Baba aingilia ishu ya Mwamnyeto Yanga

OFA mbili alizowekewa mezani na Simba na Yanga zimemchanganya, beki kisiki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto ambaye ameamua kurudi kwa Baba yake mzazi kuomba ushauri na Mzee nae kafunguka alivyomwambia.

Lakini habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba viongozi wa klabu hizo mbili wameshazungumza na Mwamnyeto huku rafiki yake wa karibu akidokeza kuwa uwezekano wa kusaini Yanga ni mkubwa.

Mtu wa karibu wa mchezaji huyo wa Taifa Stars, amelihakikishia Mwanaspoti kwamba Yanga wameipiku ofay a Simba lakini kukatokea sintofahamu baina ya mchezaji na wasimamizi wake ndio maana ikabidi akachukue ushauri wa mwisho kwa Mzee.

Simba inamtaka Bakari kwenda kuimarisha safu yao ya ulinzi haswa kwa Erasto Nyoni na Pascal Wawa huku Yanga nao wakimuangalia kama mbadala wa Kelvin Yondani ambaye kiwango chake kocha Luc Eymael hajakielewa.

Baba yake mzazi beki huyo mzee Mwamnyeto, Nondo Dosho ameliambia Mwanaspoti kuwa amefanya kikao na mwanaye huyo lakini hakuweka wazi ofa aliyomwambia.

“Nimemuita na nimezungumza naye nimemwambia sawa mimi ni baba yake lakini uamuzi utabaki kwake juu ya wapi anataka kwenda kucheza,” alisema Dosho.

“Kuna mambo mengi ya kuangalia kuna maslahi ubora wa klabu anayotaka sasa atakapoona kuna sehemu kumempa maslahi mazuri basi asaini tu wala asibubiri uamuzi wangu kwani hayo ndio mambo ya msingi.”

“Bakari atacheza kokote hilo mimi wala sina wasiwasi nalo,nimeuona ubora wake umri wake mdogo lakini ni jasiri sana hilo najivunia.

“ Pia,nimewaona mabeki wa hizo timu mbili sioni kama kuna beki anaweza kumweka benchi Bakari atacheza tu akiwa sawa kiafya sina mashaka nalo kabisa,”alisema.

“Siwezi kusema kuna timu ipi imefikia pazuri sana kwa nilivyoongea na Bakari anaona kama wanalingana itategemea wapi ataona yeye mwenyewe kunamfaa na wamefikia pale anapopataka basi amalizane nao,”aliongeza huku mchezaji huyo akigoma kuzungumza lolote kwavile yupo kwenye mkataba na Coastal Union.

Habari kutoka ndani ya Coastal zinasema vigogo hao wamekomaa kwamba mchezaji huyo hauzwi chini ya Sh100 milioni na ushee.

Habari zinasema kwamba mchezaji huyo ana mawakala wawili mmoja wa ndani na mwingine wa nje ya nchi ambao ndio wanaofanya thamani yake iwe kubwa kwavile wamemuahidi kwamba corona ikiisha kuna madili kadhaa Sauzi na Ulaya hivyo atulize mzuka.