Kigogo Yanga atoboa siri mamilioni ya usajili wa Makambo

Dar es Salaam. Aliyekuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya uchumi na fedha ya Yanga, Shija Richard ameeleza namna klabu hiyo ilivyolazimika kuchukua fedha za aliyekuwa mshambuliaji wao Heritier Makambo.
Shija katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi alieleza kuwa Yanga haikuwa na namna zaidi ya kuchukua fedha hizo Sh170 Milioni ingawa baadaye walibaini mshambuliaji huyo aliuzwa Sh250 Milioni.
“Dili la Makambo awali klabu haikuhusishwa tulistukia tu yuko na kocha Mwinyi Zahera ambaye aliomba kwenda kwao likizo baadaye ndipo wakaonekana wako na Makambo.
Shija alisema kocha Zahera aliwapigia simu na kueleza kuwa klabu hiyo iko tayari kutoa Sh 170 Milioni muda huo huo ili imnunue Makambo na kama Yanga hawataki kumuuza arudi nchini.
“Kocha alifanya vile akijua hali halisi ya kiuchumi klabuni tulikaa na kujadili hilo kilikuwa ni kipindi ambacho tulipaswa kusajili na klabu haikuwa na fedha.
“Nakumbuka kuna wachezaji kocha alikuwa amewapendekeza wasajiliwe japo wanachama na mashabiki nje hawakujua, lakini tulikuwa tunakopeshana ili kufanya usajili na tulifanya kwa mafungu.
“Kocha Zahera alipotueleza juu ya fedha hizo tulijadili mno lakini hatukuwa na namna tukamwambia awaambie hiyo klabu iweke hizo fedha kwenye akaunti ya Yanga ili zitusaidie kufanya usajili kama ambavyo kocha alipendekeza.
Alisema wakati huo mashabiki waliamini klabu ina pesa ambazo zilikusanywa na kamati ya hamasa ya klabu, lakini walikuta akaunti ya Yanga haina fedha na nyingi zilikuwa ni ahadi.
Shija licha ya wiki kadhaa zilizopita kujiuzulu ndani ya klabu hiyo ameshauri viongozi wa klabu hiyo kila mmoja kutimiza wajibu wake ili mambo yaende sawa.
Alisema yeye alijiuzulu baada ya kuona kile ambacho kinapaswa kufanyika hakiendi sawa sawa, huku kukikosekana usiri kwenye vikao vya kamati ya utendaji ambavyo walikuwa wakijadili kwa maslahi ya klabu.
“Kuna wajumbe wawili walifikia hatua ya kurekodi kwa siri sauti wakati vikao vikiendelea na kupeleka kusikotakiwa kwa nia ya kuchongeana
“Kimsingi katika vikao vya kamati ya utendaji kazi ya wajumbe ni kuhoji lakini wale tuliokuwa tukihoji tulionekana kama kuna watu tunawapinga wakati haikuwa hivyo tulikuwa na nia njema na klabu nikaona nikae pembeni,” alisema Shija.