Mkwasa apewa Yanga atangaza maangamizi upya

YANGA wamemkabidhi timu Charles Boniface Mkwassa, ambaye ataliamsha rasmi keshokutwa Jumanne huku Simba wao wakianza mambo siku ya Jumatano.
Mkwassa, ambaye yupo kwenye benchi la ufundi la Yanga, atalazimika kuliamsha kwani bosi wake, Luc Eymael amekwama kwao Ubelgiji kutokana na ndege kutoruhusiwa kutoka wala kuingia kwa sasa.
Eymael alisema kwamba; “Hata nikifanikiwa kutoka nje ya mipaka lazima nichukue usafiri wa kuunganisha sana mpaka nifike Dar es Salaam ambayo ni gharama kubwa.”
Mbali ya watani hao jadi, timu nyingine kama Coastal Union, Biashara Mara United, Mbao FC, Ndanda nazo zimepanga kuanza mazoezi baada ya sikukuu ya Eid El Fitr.
Timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) ambayo imekwisha anza mazoezi, jana walitoa likizo fupi kwa wachezaji wao kwa ajili ya sikukuu ya Eid El Fitr na wataendelea tena Jumanne.
Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mkwasa alisema wamepanga kufanya vitu tofauti na mazoea kabla ya kuanza rasmi mazoezi safari hii kwa lengo la kujiridhisha kiafya na watapambana kwelikweli uwanjani.
Alisema wachezaji watapimwa afya chini ya timu yao ya madaktari na vipimo vingine ambavyo vitafanyika kwa maelekezo ya Shirikisho la Soka (TFF), Bodi ya Ligi na serikali.
“Maandalizi yote yamekamilika, uwanja umekwisha safishwa, kambi ipo tayari na kinachosubiriwa ni sikukuu ipite na muongozo wa afya wa TFF, Bodi na Serikali
“Kwa kweli ni jambo zuri maana soka linahitaji mchezaji kutumika na kupigana kufa na kupona na atatakiwa kutumika muda wote, hivyo kujua afya zao ni suala muhimu,” alisema Mkwasa na kuthibitisha Jumanne jaramba litaanza rasmi.
Alisema kuwa wanajua kuwa ligi itakuwa ngumu kutokana na muda uliobaki na idadi ya mechi hivyo, watafanya mazoezi kwa malengo maalum.
Simba inaongoza ligi hiyo kwa pointi 71 na kufuatiwa na Azam yenye pointi 54 baada ya kucheza mechi 28 kila mmoja huku Yanga ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 51 katika mechi 27.
“Tupo nafasi ya tatu na tuna mechi moja nyuma ya Simba na Azam, hivyo tunahitaji kufanya kila linalowezekana kushinda ili kumaliza katika nafasi nzuri,” alisema Mkwasa, ambaye aliwahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Yanga.
Wakati Yanga ikitangaza kuanza na programu ya kupima afya, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema kambi yao ipo tayari na sasa wanasubiri malekezo ya kutoka mamlaka za juu.
Alisema hoteli ya kulala na uwanja wa mazoezi umekamilika na suala moja lililobaki ni kujiridhisha katika masuala ya afya za wachezaji na wanasubiri muongozo tu.
“Programu ya mazoezi yetu itategemea na jinsi ratiba itakavyopangwa, tunataka kuangalia muda uliowekwa ndio tujue nini cha kufanya, ila tutaanza mazoezi baada ya sikukuuu ya Eid El Fitr,” alisema Rweyemamu.
Lakini, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alithibitisha jana kwamba mazoezi yataanza Jumatano ila wanasubiri muongozo wa TFF. Simba ina wachezaji 23 jijini Dar es Salaam ukitoa raia wa kigeni waliokwama kwao.
Naye kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema wachezaji wake wapo mguu sawa na kutangaza kuanza kambi Jumanne.
Ligi hiyo itachezwa katika viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex na inatarajiwa kuwa na upinzani mkali huku timu zikikumbana na ratiba iliyobana sana.
Taarifa zinasema kuwa kutakuwa na mapumziko ya siku mbili kila baada ya mechi moja huku timu ambazo zipo hatua ya robo fainali ya Kombe la Azam zikibanwa zaidi kwani, zitalazimika kucheza kotekote ndani ya mwezi mmoja ili kumaliza kila kitu ndani ya muda uliopangwa.