Nyoni: Umoja wetu ndiyo mafanikio yetu

Muktasari:
Miaka 10 iliyopita, Nyoni alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars ambacho kilifuzu kwa mara ya kwanza CHAN 2009 ambayo ilifanyika nchini Ivory Coast kwa kuwang'oa Sudan.
NYOTA wa Simba, Erasto Nyoni amesema siri ya ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan, ni ushirikiano wao wa kiuchezaji kama timu huku wenye uzoefu wakiwa nyuma ya matokeo hayo.
Nyoni alisema baada ya kutanguliwa aliamini wanaweza kushinda mchezo huo hivyo akishirikiana na wazoefu wenzake, walikuwa wakiwachangamsha wachezaji wenye damu changa.
"Tuliingia kwa lengo moja tu la kuhakikisha tunafanya vizuri kwa maana ya kupata tiketi ya kushiriki CHAN, kupoteza nyumbani hakukua na maana kuwa safari yetu imeishia uwanja wa Taifa.
"Ndio maana tulivyo tanguliwa ilinibidi binafsi niwahamasishe wenzangu kuona tunakomboa lile bao kwa bahati nzuri pia tuna kocha mwenye kujua kuwapa moyo wachezaji ndio maana tuliweza kutoka nyuma," alisema.
Baada ya kusawazisha mwanzoni mwa kipindi cha kwanza, Nyoni aliona ni nafasi kwao ya kuendelea kupambana na kuona kama wanaweza kuongeza bao lingine, ambalo na kweli lilipatikana kupitia kwa Ditram Nchimbi.
Nyoni ameendelea kuwa moja ya nguzo muhimu kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa takribani miaka 10 akiwa chini ya makocha tofauti, amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho.
Upande wake Nchimbi alisema baada ya kumuona Shaaban Chilunda akiingia kwa kasi kwenye penati box aliona eneo sahihi ni kusogea kwa kipa hivyo ni kama walifanya mawasiliano ya ndani kwani alipigiwa pasi na kuunganisha.
"Niliona safari imekamilika kila ambacho tulikuwa tumekifuata tumekifanikisha, nilitazama jukwaani nikawaona mashabiki wetu wakishangilia, tukio hili nitalikumbuka," alisema Nchimbi.
Naye Juma Kaseja, alisema "Kufanya kwao vizuri nchini Sudan kumetokana na ushirikiano wao kama timu, tulikuwa tukipata moyo ya kucheza kwa kujituma kutona na sapoti ambayo tulikuwa tukiipata licha ya changamoto za hapa na pale."