Simba, Yanga kuvunja benki

KAMA kuna jambo ambalo Simba na Yanga wataonyeshana makali msimu ujao, ni usajili wa beki tegemeo wa Coastal Union na Taifa Stars, Bakar Nondo Mwamnyeto.
Kwa dau na masharti ambayo klabu hiyo ya Tanga imeweka mezani lazima kijasho kimtoke yule atakayempata mchezaji huyo vinginevyo staa huyo atapelekwa nje ya nchi kwani ana ofa kadhaa za majaribio ikiwamo Uturuki.
Iko hivi, Yanga ndio walioanza kumtaka mchezaji huyo kwenye usajili uliopita lakini wakashindwa kuvunja mkataba wake, wakaweka ishu yake pembeni.
Safari hii Simba wamejivisha mabomu na tayari asilimia kubwa wameshamalizana mambo binafsi na mchezaji huyo. Sasa kibao kimebadilika, Coastal wamebadilisha kila kitu kuhusiana na mauzo ya mchezaji huyo.
Coastal Union wanataka Simba na Yanga kupitia vigogo wao wawape udhamini wa miaka mitatu kupitia kampuni zao na hiyo itumike kama dau la kuvunja mkataba wa mwaka mmoja alionao mchezaji huyo.
Simba wakaenda mezani na Sh30milioni kwa ajili ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo, lakini viongozi wa Coastal wakagomea kwa madai kwamba ni fungu dogo sana kwani Simba ilitaka kuwadhamini kwa Sh10milioni kila mwaka.
Vigogo wa Yanga kupitia GSM wakarudi tena mezani na Sh80milioni za udhamini wa kila mwaka halafu mchezaji husika wampe Sh20milioni kila mwaka, jambo ambalo meneja wake amelikataa kwa madai kwamba mteja wake hatafaidika, atapata dau dogo sana kuliko klabu.
Mwanaspoti imeambiwa kwamba Mwamnyeto ana mameneja watatu ambao wawili wanasimamia dili zake za usajili wa ndani na mwingine nje ya nchi.
Habari zinasema kwamba meneja wa ndani ameamua kupiga kimya kuwaachia Coastal Union waendelee kujitafakari kama kweli thamani wanayotaka ndiyo halisi ya mchezaji huyo na mteja wao atanufaikaje kwani vinginevyo watamuacha hadi mkataba wake umalizike wamchukue bure.
Habari zinasema kwamba Yanga nao wamerudi nyuma na kujiuliza mara mbili kuhusiana na thamani ya mchezaji huyo mzawa wa nafasi ya ulinzi kuwa ya juu kiasi hicho na huenda wakatengua uamuzi wao wa kuendelea na usajili huo ingawa vigogo wake wanadhani wanaweza kunufaika na udhamini wa Coastal kama klabu kirahisi.
Pamoja na kiongozi wa Coastal Union, Steven Mguto kutopokea simu yake kuhusiana na sakata hilo, mmoja wa mameneja wa Mwamnyeto, Kassa Mussa alithibitisha mchezaji huyo kufuatwa na klabu hizo mbili lakini hakuna lililoafikiwa.
Alisema kuwa mbali na watani wa jadi, pia kuna timu za Ubelgiji na Ugiriki ambazo nazo zinamuhitaji Mwamnyeto ambaye ameonyesha kiwango kikubwa katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
LAZIMA KIELEWEKE
Lakini kwa nyakati tofauti licha ya kutotaka kutaja jina la mchezaji wanayemuwania, lakini wakubwa wa Simba na Yanga wamesisitiza kuwa hawawezi kumshindwa mchezaji yeyote mzawa anayetakiwa na kocha.
Ofisa Mtendaji wa Simba, Senzo Mazingisa amesema mchezaji yeyote mzawa ambaye watakuwa na mahitaji naye watamsajili kwani lengo lao ni kupata timu imara inayonyumbulika.
Senzo alisema hilo linaanzia katika wachezaji wa hapa ndani kwa maana ambao wapo katika klabu za Ligi Kuu Bara, kama kuna ambaye yupo katika orodha ya mahitaji ya kocha wao, Sven Vandenbroeck basi watamsajili.
“Kama kocha atakuwa anamtaka mchezaji yeyote wa hapa ndani kulingana na mahitaji yake basi hakuna ambaye tutamkosa na kama ukiona kuna mchezaji wa ndani tumeshindwa kumsajili basi ujue hakuwa katika malengo yetu,” alisema Senzo ambaye ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika.
“Nguvu na ushindani wetu katika usajili tunakwenda kushindana kwa wale wachezaji ambao wanatoka nje ya Tanzania,” aliongeza Senzo ambaye Mwanaspoti inajua kwamba tayari ameshawapa majukumu kadhaa mawakala wakubwa wa Afrika kumchekia mashine za maana na kumpa mapendekezo yao.
Yanga kwa upande wao, Mkurugenzi wa GSM, Hersi Said amesema hata wao wamejipanga na hawatashindwa kumchukua yeyote wanayemtaka.
Hersi alisema kabla ya kocha wao, Mbelgiji Luc Eymael kuondoka nchini aliacha mapendekezo akitaka yafanyiwe kazi katika usajili na kuna wachezaji ambao wapo ndani ya kikosi ametaka waongezewe mikataba.
IMEANDALIWA NA MAJUTO OMARY, THOBIAS SEBASTIAN NA MWANAHIBA RICHARD