Beki aeleza kisa cha Nyoni

KIUNGO Baraka Majogolo amemtaja, Erasto Nyoni, kuwa ndiye mchezaji anayempa maujanja na anaamini kama ataendelea kuyashika atafika mbali.
Majogolo mchezaji wa Polisi Tanzania na Taifa Stars na sasa kuna tetesi timu maarufu za Simba na Yanga zimeanza kuwinda saini yake kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji kwa ubora pamoja na beki ya kati na kiungo mshambuliaji.
Amesema, amekuwa akimfuatilia kwa ukaribu Nyoni ndani na nje ya uwanja kuona namna anavyofanya na kujifunza mambo mengi.
"Nyoni ni mchezaji ambaye nimekuwa namfuatilia kwa karibu, najifunza mambo mengi kutoka kwake ya ndani na nje ya uwanja. Unapozungumzia ndani ya uwanja ni namna anavyocheza, kwanza ni kiranja ndani ya uwanja kutokana na namna anavyoongoza na kusaidiana na wenzake, anatumia akili, nguvu kidogo, anajua kucheza mpira wa chini na juu pia, kukaba, kushambulia, naweza kusema kila kitu,"alisema Majogolo ambaye alikipiga Ndanda FC pamoja na Tanzania Prisons miaka ya nyuma.
"Upande wa nje ya uwanja, jamaa ana busara na mara nyingi ninapokuwa nazungumza naye amekuwa akinishauri mambo mengi mazuri na kunitia moyo, niongeze bidii katika kazi yangu."
Alisema, jicho lake lazima liangalie kwake kwa sababu ni mchezaji anayependa kuona unafanikiwa, ni kama kaka na mcheshi.
BOBAN, YONDANI WAHUSIKA
Majogolo ameongeza kusema, awali kabla ya kiungo, Haruna Moshi 'Boban' hajastaafu ndiye mchezaji aliyekuwa anapenda staili ya uchezaji wake: "Boban ndiye mchezaji aliyekuwa kichwani zaidi hapo awali, lakini tangu atoke kwenye medali ya soka mtu ninayemfuatilia ni Nyoni."
"Pia, Yondani (Kelvin) amekuwa kama kaka kazini, amekuwa akinishauri mambo mengi mazuri na namna natakiwa kufanya ili nifanikiwe katika kazi yangi,"alisema Majogolo.
Alisema, wapo wachezaji wengine ukiachana na Nyoni, Boban, Yondani kama Juma Kaseja, kutokana na ukongwe wake kwenye soka, amekuwa akipata vitu vya kujifunza kutoka kwake.