Carlinhos: Sasa Naanza mambo

KIUNGO nyota wa Yanga, Carlinhos amewaambia viongozi kwamba; “Sasa ndio mtaona makali yangu.” Kwa mujibu wa Hersi Said ambaye kigogo wa GSM, “ametuhakikishia mwenyewe kwamba sasa anaanza mambo.”
Yanga ilitua mkoani hapa jana wakiwa na msafara wa watu 40 tayari kuikabili Mtibwa Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu Kesho Jumapili.
Lakini Carlinhos ambaye ni raia wa Angola, tangu atue nchini amekuwa katika wakati mgumu kupata chakula ambacho amezoea na vinavyompa nguvu uwanjani.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya kambi ya Yanga, hakuna chakula cha Kitanzania ambacho ameweza kukizoea hatua ambayo imezidi kumpa wakati mgumu kurejea katika ubora wake achilia mbali kukaa kwake nje kwa miezi mitano kutokana na Covid 19 huko kwa Angola.
Inaelezwa kwamba kiungo huyo amekuwa akiishi katika wakati mgumu kujaribu kuzoea vyakula vya hapa nchini ambapo angalau pizza pekee ndio alikuwa anaona anaweza kujaribu.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said alisema kutokana na hali hiyo tayari wamepata mpishi maalum atakayekuwa anamtengenezea kiungo huyo chakula.
Hersi alisema walilazimika kufika mpaka ubalozi wa Angola nchini ambao nao waliwapa ushirikiano wa kumpata mtu huyo ambaye sasa sio tu atakuwa anamtengenezea chakula bali atawapa ujuzi wapishi wao wa klabu.
“Tumefanikisha hilo kwanza tunashukuru sana wenzetu wa ubalozi wa Angola ambao walitupa ushirikiano mkubwa tangu tupate changamoto hii ya vyakula kwa mchezaji wetu,” alisema Said.
“Kwasasa tayari mtaalam huyo wa mapishi ameshaanza kazi yake atakuwa akifanya hiyo kazi lakini pia atakuwa akiwapa ujuzi huo wenzake ambao wanatutengenezea vyakula wachezaji wetu kule kambini.
“Unajua kwanza Carlinhos amevumilia sana na alikuwa anashindwa kuonyesha ubora wake halisi kutokana na changamoto hii, kama unavyofahamu mpira ni mchezo wa mazoezi makali sasa ni lazima uweze kula vizuri lakini sasa mambo yatakuwa sawa.
“Tunafahamu ubora wa Carlinhos na tuwaambie mashabiki wetu baada ya muda kuanzia sasa watamjua vyema mchezaji huyu na hilo ametuhakikishia mwenyewe,” alisema Hersi na kuongeza kwamba anaridhika na hali ya mambo ndani ya klabu hiyo huku akitoa pia rai ya mashabiki kumuachia kocha Zlatko Krmpotic kufanya kazi yake.
Yanga itawakabili Mtibwa kuanzia saa 10:00 kesho Jumapili.