Dk Msolla atolea ufafanuzi kauli ya kuchangia wachezaji

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema hadi sasa usajili wa wachezaji wa kigeni nane umekamilika na suala la wanachama kuchangia ni nafasi mbili zilizobaki ili kukamilisha idadi ya 10.
Wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Mwananchi mjini Dodoma Agosti 22 alisema wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanatakiwa kuchangia ili kufanikisha usajili wa nyota wawili wa kigeni.
Kauli hiyo imeibua gumzo mtandaoni wananchi wakitaka kujua kama hao wawili ni miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja nchini Muangola Fernandes Guimares na Yacouba Sogne.
Kikosi cha Yanga kiliwabakisha nyota watatu kipa Faruk Shikhalo, Haruna Niyonzima na beki kisiki Lamine Moro huku waliowasili kuungana na wenzao hadi sasa ni Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda na Michael Sarpong.
“Tuna nafasi mbili zimebakia ili wafike 10, tuliona kama uongozi tumpe nguvu mdhamini wetu, watu wachangie tukamilishe hao wengine. Hao wawili sio wale ambao tushamalizana nao. Kama hatutafanikisha kwenye usajili huu mkubwa kuna dirisha dogo tutamaliza” amesema Msolla
Dk Msolla ametolea mfano wa mwaka jana wananchi walichanga kusajili wachezaji 10 basi na safari hii wafanye hivyo kwa nafasi mbili.
Kuhusu mkataba wa La Liga na Sevilla, Dk Msolla amesema mwisho wa mwezi huu watapata andiko la kwanza la mfumo tarajiwa wa kuendesha klabu na kitachofuata ni kubadilisha katika ya Yanga.
“Mwisho wa mwezi huu tutapata andiko la kwanza, tutaitisha mkutano mkuu wa matawi kuwapitisha kwenye andiko la kwanza la katiba pendekezwa na muundo pendekezwa kisha waende kwenye matawi wakajadili kwa wiki tatu” amesema Msolla
Dk Msolla ameongeza kuwa rufaa ya sakata la Morrison kwenda Fifa na leo watawasilisha Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kuona wataamuaje.
Katika mkutano huo Dk Msolla amemtambulisha Senzo Mazingisa kuwa mshauri katika timu hiyo kwenye mabadiliko ya muundo wa klabu ambao unahusisha La Liga na Yanga.
Senzo amesema anafuraha kufanya kazi Jangwani yenye rekodi nyingi na atahakikisha anashiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko na kuleta matokeo chanya.