Karia aeleza mafanikio ya uongozi wake

Muktasari:
"Utawala umekuwa ni wa wazi na huwa siingilii kamati za TFF naziacha huru ili zifanye kazi kwa kuzingatia kanuni husika hilo kinakwenda sawa,"amesema.
RAISI wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amesoma hutoba mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi, Damas Ndumbaro akielezea mafanikio waliyoyapata katika uongozi wake.
Karia amesema kwa sasa soka la Tanzania limepiga hatua kubwa akiamini ndio sababu ya yeye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Cecafa.
Amesema bila mafanikio kuwepo ingekuwa ngumu yeye kupewa dhamana ya kuiongoza Cecafa na kwamba yote hayo yanatokana na ushirikiano wa wajumbe.
"Kuna mabadiliko makubwa tangu niingie madarakani 2017 tumechukua makombe nane ya mashindano tofauti, tunasimamia timu zote za Taifa ipasavyo,"
"Utawala umekuwa ni wa wazi na huwa siingilii kamati za TFF naziacha huru ili zifanye kazi kwa kuzingatia kanuni husika hilo kinakwenda sawa,"amesema.
Mbali na hilo amesema katika utawala wake ameboresha usimamizi wa fedha ili kuhakikisha mapato na matumizi yanakuwa wazi.
"Namna ambavyo tunasimamia mapato kwa uwazi tumekuwa mfano kwa Afrika sisi na wenzetu Eltrea na kufanya nchi nyingine ziweze kutuiga,"amesema.
VIWANJA KUBORESHWA
Karia amesema tayari wamewasiliana na viongozi wa serikali kupitia chama tawala cha CCM kuhakikisha wanakarabati ili kuboresha maendeleo ya soka.
"Tunataka kukarabati viwanja kama 10 tunawasiliana na Halmashauri za mikoa ili kuvikarabati ili timu ziweze kucheza sehemu zinazostahiki,"amesema.