Makambo Kalitibua

Muktasari:
- Mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo anazidi kuwapa presha na kuawanyima raha mabeki wa timu pinzani kasi ya Mkongo huyo wa Yanga katika kufumania nyavu imezidi kuwashtua wengi kwasababu amekua straika ambaye ukizubaa kidogo tu, lazima akulize.
ELIUD Ambokile wa Mbeya City ndiye anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji mabao wa Ligi Kuu Bara, lakini kama kuna straika anayewanyima raha na kuhofiwa kwa sasa na mabeki wa timu pinzani basi ni Heritier Makambo wa Yanga.
Kasi ya Mkongo huyo wa Yanga katika kufumania nyavu imewapa presha kubwa mabeki na makipa wa timu pinzani katika mechi hizi za duru la kwanza kwa vile ni straika mjanja mjanja ambaye ukizubaa kidogo tu, lazima akulize.
Kwa sasa mabeki na makipa wanakabiliwa na kazi kubwa ya kufanya kumdhibiti Makambo ambaye kasi yake ya kufumania nyavu inaonekana kuwashinda idadi kubwa ya mabeki wa timu za Ligi Kuu.
Nyota huyo ameshafunga mabao nane dhidi ya timu nane tofauti kati ya 15 zilizocheza na mabingwa hao wa kihistoria, huku akiwa ni mshambuliaji pekee kufanya hivyo katioka ligi ya msimu huu mpaka sasa akimfunika hadi Ambokile.
Makambo amefunga mabao yake dhidi ya Mtibwa Sugar, Coastal Union, Alliance, Lipuli, Mwadui FC, Kagera Sugar, JKT Tanzania na kisha kumalizia kwa Biashara.
Katika mechi 15 ambazo Yanga imecheza hadi sasa ni timu saba tu ambazo Makambo alishindwa kufumania nyavu zao ambazo ni Simba, Prisons, Stand United, KMC, Mbao FC, Ndanda FC na Singida United.
Kutokana na kasi hiyo ya upachikaji mabao, straika huyo sasa ananyemelewa na vita kubwa dhidi ya mabeki wa timu nne ambazo Yanga bado haijacheza nazo kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu ambazo ni wazi hawatokuwa tayari kumruhusu aendeleze makali yake.
Mabeki wa shoka ambao wataanza kukabiliana na kibarua cha kuzima mziki wa Makambo ni Renatus Morris na Tumba Swedi wa Ruvu Shooting ambayo ndio itacheza na Yanga kwenye mchezo unaofuata wa Ligi Kuu, yaani Jumapili hii tu.
Baada ya shughuli baina ya ukuta huo wa Shooting na Makambo, safu ya ulinzi ya Mbeya City inayoundwa na nahodha Erick Kyaruzi na Ally Lundenga nayo itakuwa majaribuni dhidi ya straika huyo mwenye uwezo wa kufunga mabao ya vichwa na yale ya mguu.
Mshambuliaji huyo baada ya kumalizana na Mbeya City, atahamisha makali yake dhidi ya African Lyon ambapo atakabiliana na mabeki Agustino Samson na Daud Mbweni wanaounda safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Shughuli ya aina yake itakuwa kwenye mchezo wa mwisho wa duru la kwanza ambao Yanga itacheza dhidi ya Azam ambapo Makambo atakuwa na shughuli ya aina yake dhidi ya ukuta wa chuma unaoundwa na mabeki visiki wa kati, Aggrey Morris na Yakub Mohammed.
Pengine mechi hiyo ikawa moja ya vipimo vigumu kwa Makambo kwani ukuta wa Azam ni miongoni mwa safu ngumu za ulinzi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita tu.
Ukiondoa mabeki hao wa timu hizo nne, bado mabeki wa timu nyingine saba ambazo Makambo hakuzifunga mzunguko wa kwanza, wanapaswa kujipanga kikamilifu pindi watakapokutana na straika huyo ili kumdhibiti asitanue rekodi yake ya kuzifunga idadi kubwa ya timu msimu huu.
Msikie Jembe Ulaya
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema kinachombeba Makambo ni udhaifu wa mabeki ingawa mshambuliaji huyo hana makali ya kumfanya aogopwe.
“Binafsi kwa mtazamo wangu, Makambo ni mchezaji mwenye uwezo wa kawaida ila shida kubwa inakuja kwamba mabeki wetu wanaocheza kwenye ligi yetu, uwezo wao uko chini hivyo ndio maana anawafunga. Lakini kiuhalisia Makambo sio aina ya mshambuliaji mwenye uwezo wa kupambana pindi anapokutana na mabeki wazuri tofauti na mtu kama Obrey Chirwa,” alisema.