Mpepo apiga tizi mlimani

Muktasari:
Mpepo ambaye alirejea nchini akitokea Msumbiji ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhari ya corona akiwa Tanzania , aliwahi kucheza Ligi Kuu Bara kwa vipindi tofauti akiwa na klabu ya Tanzania Prisons na Singida United.
STRAIKA Mtanzania, Eliuter Mpepo anayecheza kwa mkopo soka kulipwa klabu ya CD Costa Do Sol nchini Msumbiji, ameendelea kujiweka fiti akiwa nchini kwa kufanya mazoezi ya kupanda na kushuka mlima.
Nyota huyo wa A.D. Sanjoanense ya Ureno, amesema sababu ya kufanya mazoezi ya namna hiyo ni kutaka kulinda utimamu wake wa mwili ili janga la corona litakapopita arejee Msumbiji akiwa fiti.
"Nimejipangia mazoezi tofauti ya kufanya ambayo ninaamini yatanisaidia. Kupanda na kushuka najijengea pumzi na stamina miguuni, nafanya hivi kwa sababu ndani ya huu msimu natakiwa kuonyesha.
" Nikifanya vizuri itakuwa rahisi kwangu kwenda Ureno na kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza kwa sababu huwa wananifuatilia," amesema mshambuliaji huyo.
Akimaliza mazoezi ya kupanda mlima ambayo amekuwa akifanya asubuhi, Mpepo ambaye aliwahi kuichezea Buildcon ya Zambia, amesema hufanya mazoezi ya kuuchezea mpira huku akinyoosha viungo.
Aina hayo ya mazoezi amesema amekuwa akiyafanya kwa kiasi ili kuepuka mwili kukakamaa na kushindwa kufanya kiwepesi vitu ambayo anatakiwa kufanya huku viungo vikiwa katika hali ya kawaida.
CD Costa Do Sol ambayo anaichezea kwa mkopo Mpepo ni mabingwa wa Msumbiji hivyo nanafasi ya msimu ujao kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika.