Mpepo atoboa siri za Zesco kwa Yanga

Muktasari:
Were ndiye aliyeibeba ZESCO United ugenini kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Green Mamba kwa kufunga bao pekee lililowafanya watinge raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-0 kutokana na mchezo wa kwanza wakiwa kwao Zambia kushinda kwa mabao 2-0.
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Kitanzania, Eliuter Mpepo anayeichezea Buildcon ya Zambia, amewastua mapema Yanga wajiandae kuwadhibiti Were Jesse, Kasumba Umar na Ching’andu John wa ZESCO United kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga wataanzia nyumbani uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania nafasi ya kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ZESCO United kati ya Septemba 13 hadi 15.
Mpepo alisema baada ya kuondoka kwa Lazarous Kambole, Were, Kasumba na Ching’andu wamekuwa wakitegemewa kwenye kikosi cha ZESCO United ambayo inanolewa na kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina.
“Mchezaji wao tegemeo msimu uliopita alikuwa Kambole ambaye amejiunga na Kaizer Chiefs, naona kuondoka kwake kumetoa nafasi kwa Were kuwa ndio staa wa timu yao huku wanamwita mfalme.
“Anajua namna ya kuulinda mpira, huwa tunatumia uwanja mmoja wa mazoezi baina ya timu yangu ya Buildcon na ZESCO kuna siku tuliwahi kufika ilibidi tusubiri wamalize program zao, alikuwa akiwasumbua sana wenzake, ni mwepesi wa uamuzi,” alisema Mpepo.
Mshambuliaji huyo wa Kitanzania aliongeza kwa kusema, Were na Kasumba ni washambuliaji, lakini Ching’andu ni kiungo mchezeshaji mwenye uwezo pia wa kufunga.
Akizungumzia udhaifu wao, Mpepo alisema ZESCO United wanapitika pembeni kama Yanga watakuwa na mawinga wenye kasi basi ni rahisi kufungika kupitia maeneo hayo.