Senzo ahojiwa polisi, aachiwa

MSHAURI wa Klabu ya Yanga, Senzo Mazingisa leo Jumatano Novemba 11 amehojiwa na maofisa polisi kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ya kijamii imeeleza kwamba sababu za Senzo kuhojiwa ni kuwepo na tuhuma za mawasaliano yake na aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanachama wa Simba, Hashim Mbaga.
Hivi karibuni Mbaga aliwekwa ndani akituhumiwa uwepo na mawasiliano na Senzo ambayo yalilenga kuihujumu Simba sababu ambayo ndiyo inayodaiwa hata mshauri huyo kuhojiwa na Polisi.
Senzo aliwahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba ambapo alijiuzulu nafasi hiyo na kwenda kuajiriwa na mahasimu wa klabu hiyo, Yanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Edward Bukombe amekiri kuhojiwa kwa Senzo kituoni hapo.
"Ni kweli leo Senzo aliitwa kwa ajili ya kuhojiwa na alishaachiwa muda mrefu, aliohojiwa na idara ya upelelezi bado hawajanipa mrejesho zaidi mpaka sasa," amesema RPC Bukombe.