Wawili wapewa namba ya Mkude Simba
KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kuumia na kukosekana kwa Jonas Mkude ambaye kwa wiki mbili atakuwa nje ya uwanja, kwa vile kikosini kwake ana mashine za maana akiwamo Mzamiru Yasin na Mbrazili, Gerson Fraga.
Sven alisema nyota hao wawili ameshawaandaa kuziba nafasi ya Mkude aliyeumia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya KMC, katika pambano lao la kesho dhidi ya Ruvu Shooting na nyingine zilizopo mbele yao.
Kocha Sven amesema wakati wanamuombea kiungo huyo aimarike na kurudi uwanjani kuungana na wenzake, kukosekana kwake kutatoa nafasi kwa mchezaji mwingine.
“Simba ina kikosi kipana, naweza kumtumia Mzamiru akipokezana na Fraga kipindi hiki,” alisema kocha huyo Mbelgiji.
Akizungumzia maendeleo yake, Mkude alisema japo maumivu yameanza kupungua, lakini bado hayuko sawa.
“Kiasi fulani maumivu yamepungua, nimefanya vipimo na matibabu yangu yamekwenda vizuri, siko poa sana, vidole vya mguu wangu wa kulia vyote viliumizwa,” alisema Mkude mchezaji mwandamizi wa Simba katika kikosi cha sasa akikipiga tangu 2010.
Mkude alisema anaendelea na matibabu kama ambavyo madakatari wameelekeza na anaamini ndani ya muda aliotakiwa kuwa nje ya uwanja ataimarika.
“Nilikuwa katika maumivu makali hasa siku ya kwanza na ya pili tangu nilipoumia (Jumatatu na Jumanne), nashukuru Mungu matibabu yangu yamekwenda vizuri, vidole vyote vya mguu wangu wa kulia vilipata shida,” alisema.
Naye Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema Mkude atakuwa nje kwa wiki mbili akiwa katika uangalizi maalumu akiendelea na matibabu na kufanya mazoezi mepesi.
“Tunaendelea kumhudumia ili baada ya hizo wiki mbili awe ameimarika na aweze kurudi kuendelea na mazoezi kama kawaida na kuungana na wenzake,” alisema Dk Gembe.
Kuwa nje kwake kwa wiki mbili ina maana Mkude anaweza kuibukia kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Azam, lakini akikosa mechi tatu za Ligi Kuu ikiwamo wa Jumapili dhidi ya Ruvu, ile ya Mwadui na Mbeya City.
Dk Gembe alipoulizwa tatizo hasa nini kwa Mkude, alisema masuala ya ugonjwa ni siri ya mgonjwa mwenyewe, lakini kwa sasa kiungo huyo hajambo kiasi na wanaendelea kumhudumia ili aimarike ndani ya wiki hizo mbili.
Mkude alikanyangana na Kijili wakiwa katika harakati za kuwania mpira, ambapo Kijili alisema aliudokoa mpira huo na Mkude akapiga vidole vyake chini ya meno ya viatu vyake kuumia, ingawa yeye pia aliumia nyayo za mguu wa kulia, lakini si kwa kiasi kikubwa na alivumilia hadi mwisho wa mchezo.
“Nia ilikuwa tuchukue mpira, mimi nikamuwahi, sikumchezea rafu, ‘niliuchopu’ mpira bahati mbaya yeye akaingiza mguu kwenye meno, akapata shida kwenye vidole,” alisema Kijili.
Katika mchezo huo wa Jumatatu iliyopita, Mwamuzi Said Pambalelo alisimamisha mpira ili kuruhusu Mkude apewe huduma ya kwanza kabla ya madaktari wa Simba kumtoa nje na kuendelea kumpa huduma ya kwanza kisha wakaita gari la wagonjwa.