Yanga yajifungia Uwanja CCM Kirumba ikijianda kwa Pyramids

Muktasari:

Mashabiki na Wanachama wameonekana kuwa katika na vikundi vya hapa na pale wakiweka mikakati thabiti ya kuwanyoosha Pyramids katika mchezo wa Jumapili

Mwanza. Uongozi wa Yanga umezuia mashabiki na wanahabari kuingia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kushuhudia mazoezi ya timu hiyo.

Uamuzi huo wa Yanga unatokana na maelekezo ya Kocha Mwinyi Zahera kutotaka uwazi katika mazoezi yao ya kujianda na mchezo wao dhidi ya Pyramids katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Mashabiki walijitokeza waliishia mlangoni, huku makomandoo hao wakisisitiza kutoruhusu mtu yeyote kuchungulia mazoezi hayo.

Hata hivyo baadaye wanahabari waliruhusu kuingia uwanjani kwa dakika chache kwa ajili ya kuchukua picha na kuondoka.

Mashabiki wajipanga Mwanza

Vikao vya mashabiki na Wanachama wa Yanga vimetawala wakati timu yao ikiendelea na mazoezi.

Mashabiki na Wanachama wameonekana kuwa katika na vikundi vya hapa na pale wakiweka mikakati thabiti ya kuwanyoosha Pyramids katika mchezo wa Jumapili ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

"Yaani hapa ni presha tu, tunataka heshima Jumapili, hapa ni Mwanza lazima Waarabu wafe, tumejipanga kwa kila mbinu" alisema shabiki wa Yanga, Ghalib Fadhir.