Zahera ampeleka Molinga Morocco

Muktasari:

  • Molinga hadi sasa ameifungia Yanga mabao nane katika Ligi Kuu Tanzania Bara na ndiye mchezaji wa timu hiyo aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika msimu huu.

Dar es Salaam. Mshambuliaji anayeongoza kwa mabao Yanga, David Molinga Falcao yuko mbioni kutimkia Morocco baada ya Ligi Kuu nchini kumalizika.
Molinga anakaribia kujiunga na klabu ya Renaissance Sportive de Berkane.
Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameithibitishia Mwanaspoti juu ya mpango huo.
Zahera ambaye ndiye alimleta Molinga Yanga kabla ya kuondoka na kumuacha amesema dili la mchezaji huyo liko mbioni kukamilika na msimu ujao atacheza soka la kulipwa nchini humo.
Zahera aliwahi kukaririwa na gazeti la Mwanaspoti akieleza kuwa mchezaji huyo hana furaha kucheza Yanga.
"Kila kitu kinakwenda vizuri, anachosubiri ni kumaliza mkataba wake na Yanga ili kuanza maisha mapya ya kisoka Morocco," alisema.
Ingawa mshambuliaji huyo alipotafutwa kuzungumzia mipango hiyo, simu yake haikupatikana.