Bodi ya Ligi: Tumechukua  tahadhari Kimbunga Hidaya

Mwelekeo wa Kimbunga Hidaya

Muktasari:

  • Mechi za ligi zitaendelea kama kawaida kwa kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania haijaelekeza vinginevyo juu ya shughuli mbalimbali kuzuiwa, badala yake imetaka watu kuwa makini na mabadiliko hayo

MWANDISHI WETU
BODI ya Ligi Tanzania (TPLB) imesema imechukua tahadhari muhimu juu ya tishio la kimbunga kinachoendelea kinachojulikana kwa jina la Hidaya.

Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda amesema kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juu ya tishio la kimbunga hicho kwa upande wao wamechukua hatua kuhakikisha mechi zinazoendelea zinachezwa kwa usalama na tahadhari.

Boimanda amesema bodi inaendelea na mawasiliano ya mara kwa mara na TMA ili kupata taarifa muhimu za mabadiliko ya hali ya hewa nchini.

"Ilipotoka tu taarifa hiyo hatua za haraka tulichukua kwanza kujua namna kimbunga hicho kinavyoweza kuwa ukizingatia mechi za ligi zinachezwa viwanjani maeneo ambayo ni ya wazi, lakini bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa hali ya hewa kujua kila hatua ya mabadiliko ya hali ya hewa hasa maeneo ambayo yametajwa kwamba kunaweza kutokea," amesema Boimanda.

"Hatua ya pili ni kuchukua tahadhari. Tumeshajipanga kote ambako mechi zinachezwa kwa wasimamizi wa michezo kuhakikisha wanakuwa makini na mabadiliko ya hali ya hewa na kama ikitokea hali yoyote, basi mawasiliano ya haraka yafanyike kwa bodi ili hatua za haraka zichukuliwe."

Boimanda amesisitiza kuwa mechi za ligi zitaendelea kama kawaida kwa kuwa TMA haijaelekeza vinginevyo juu ya shughuli mbalimbali kuzuiwa, badala yake imetaka watu kuwa makini na mabadiliko hayo.