Ishu ya Manji kurejea Yanga ipo hivi

Muktasari:

  • Manji alikuwa Uwanja wa Mkapa Jumamosi iliyopita akiishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na kukaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kufikisha pointi 58 kwenye michezo 22.

Mwenyekiti na mfadhili wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji amesema kwa sasa hafikirii kurejea ndani ya klabu hiyo ingawa anafurahia kuona imekuwa na umoja na mshikamano wa hali ya juu.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Manji alisema kwa sasa umri wake unambana kujiweka karibu na timu hiyo na soka kwa ujumla, hivyo anaendelea kujishughulisha na mambo mengine.

“Kwa sasa siwezi, kwanza umri umeenda siwezi zile pilikapilika za kusimamia timu,” alisema Manji aliyeiongoza Yanga kwa miaka minne.

“Unajua hata kama utakuwa ofisini, tabia yangu ni kwamba napenda kufanya kazi zote nikiwa karibu. Naweza kuwa na viongozi wengine lakini nitalazimika kusafiri na wachezaji, nahakikisha kila kitu chao kinaenda vizuri, ukweli kwa kipindi hiki sitakuwa na uwezo tena wa kufanya hivyo wanatakiwa kufanya vijana.”

Manji alisema kuwa pamoja na hilo, anafurahia kuona klabu hiyo ina umoja wa hali ya juu kwa sasa jambo ambalo lilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu.

“Moja ya jambo ambalo nakumbuka nililifanya na kuisaidia Yanga hii kufika hapa ni kuweka umoja, wakati naingia nilikuta migogoro mingi kulikuwa na makundi matatu, nakumbuka moja liliitwa Yanga Asili, lingine Yanga Kampuni na moja liliitwa Yanga Akademia.

“Nilitumia ushawishi wangu wote na kuhakikisha haya makundi yanaisha na Yanga ikasimama, nafikiri imewasaidia hadi leo ndiyo maana kuna umoja,” alisema Manji,” alisema Manji.
Manji alisema kwake alitanguliza maslahi ya Yanga na soka mbele kwa vile mchezo wa mpira wa miguu unashikilia furaha ya wengi.

“Nilianzisha mfumo wakati mwingine wa kununua tiketi zinaenda kugawiwa kwenye matawi ya Yanga kwa kuwa nilitaka kurudisha kwa jamii. Kama unakumbuka mchezo wa Yanga na TP Mazembe kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza mashabiki waliingia bure.

“Pale haikuwa bure kama ambavyo inafanyika sasa bali nilinunua tiketi zote zikagawiwa kwa mashabiki wa Yanga kupitia kwa viongozi wa matawi yao. Nia ilikuwa ni kuhakikisha mchezo huu unarudi kwa jamii yetu,” alisema Manji mmoja wa wafadhili wa klabu walioweka rekodi ya kuwa kipenzi cha mashabiki nchini.

Chini ya uongozi wa Manji, Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne huku ikitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja.

Bilionea huyo anakumbuka na wengi kwa usajili wa wachezaji mastaa wa ndani na wale waliokuwa wakitamba Afrika Mashariki na Kati.