Kanuni yaiweka pabaya USM Alger

Muktasari:

  • Mechi za marudiano za hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika zimepangwa kuchezwa Aprili 28 ambapo timu zitakazoingia fainali zitaumana katika mechi ya kwanza itakayochezwa Mei 12 na marudiano itakayochezwa Mei 19.

Wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) likisubiriwa kutoa uamuzi wa mechi iliyoshindwa kuchezwa ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya USM Alger na RS Berkane, kanuni za mashindano hayo huenda zikaiumiza USM Alger iliyokuwa mwenyeji wa mechi hiyo.

Mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa Aprili 21, haikufanyika baada ya RS Berkane kugomea kufuatia kitendo cha kuzuiliwa kutumika kwa jezi zao zilizokuwa na ramani na bendera ya nchi yao ya Morocco.

Serikali ya Algeria iliwazuia Berkane kutumia jezi hizo na kuwalazimisha kuzitumia nyingine ambazo hazikuwa na bendera wala ramani ya Morocco jambo lililosababisha mechi hiyo kutofanyika baada ya wageni kukataa kuzitumia.

Kanuni ya 11 ya mashindano hayo ibara ya tatu, inafafanua kuwa mchezo ambao utavunjika kutokana na vitendo vya usumbufu kwa wageni, timu mwenyeji itahesabika kupoteza mechi na itaondolewa mashindanoni.

"Kama refa atalazimika kusimamisha mechi kabla ya kumalizika kwa muda wake wa kawaida kwa sababu ya uvamizi wa eneo la kuchezea au vurugu dhidi ya timu mgeni, timu mwenyeji itapoteza mchezo na kuondolewa mashindanoni," inafafanua kanuni hiyo.