Mastaa sita Simba wanavyoibeba Yanga

Muktasari:

  • Ndani ya kikosi cha Yanga kuna mastaa sita ambao waliwahi kutajwa kutakiwa na Simba lakini ghafla watani wao wakajibebea kiulaini na sasa wanasaidia kupeleka maumivu kwa wekundu hao.

WAKATI mashabiki wa Simba wakiendelea kulia na mastaa wa kikosi chao baada ya timu yao kukosa matokeo mazuri lakini upande wa pili umefichua juu ya sajili sita nzito za wekundu hao zinazowabeba watani wao Yanga.

Ndani ya kikosi cha Yanga kuna mastaa sita ambao waliwahi kutajwa kutakiwa na Simba lakini ghafla watani wao wakajibebea kiulaini na sasa wanasaidia kupeleka maumivu kwa wekundu hao.


YAO KOUASSI

Dirisha kubwa la usajili lililopita beki Attohoula Yao alikuwa kwenye listi ya Simba kama ingizo jipya lililotakiwa kuja kuongeza nguvu ndani ya kikosi cha wekundu hao baada ya kumshuhudia akiwa na klabu yake ya ASEC Mimosas iliyokutana nao mara mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilikuwa na hesabu za kumchukua Yao lakini baadaye wakabadilisha akili na kumchukua beki wa ndani, David Kameta 'Duchu' kisha baadaye Yanga kuvamia na kupita na beki huyo ambaye ametokea kuwa 'mtu sana' pale kwenye ukuta wa chuma wa timu ya Wananchi huku akiwa na msaada mkubwa katika mashambulizi kutokana na kupiga krosi zinazoleta matatizo mengi kwa wapinzani akifunga bao moja na kutoa asisti saba na mpaka sasa ndiye kinara wa asisti kwa mabeki katika ligi nzima.

MUDATHIR YAHYA

Simba ilidaiwa ilishafanya mazungumzo ya kila kitu na kiungo Mudathir Yahya mara tu baada ya kumaliza mkataba wake na Azam FC kisha kurudi kwao kupumzika kwa miezi kadhaa akiwa hana timu.

Haikuwa na shida tena kwa Simba kumalizana na kiungo huyo kwa kuwa hakuwa na mkataba wowote na klabu yake lakini Wekundu wa Msimbazi wakazembea kidogo tu kabla ya Yanga kuingia msituni na kutumia siku tatu tu kumchukua akiwa kama mchezaji huru na wikiendi iliyopita alikuwa na dakika 90 za pili za ushindi akiwa na timu yake mpya dhidi ya wekundu hao msimu huu.

NICKSON KIBABAGE

Wakati beki wa kushoto Nickson Kibabage akianza kuwa na kiwango bora akiwa na klabu ya Singida Fountain  Gate, Simba ilifikiria kumchukua beki huyo kuja kusaidiana na nahodha wao msaidizi Mohammed Hussein 'Tshabalala' lakini baadaye kosa lile lile likafanyika, Yanga ikamuwahi na kumchukua kwa mkopo.


STEPHANE AZIZ KI

Kila mara kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz KI anapofunga bao dhidi ya Simba au dhidi ya timu yoyote, mabosi wa wekundu hao watakuwa wanapata maumivu mara mbili kwa kujua kwamba angekuwa mchezaji wao kwani klabu hiyo ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumfuata staa huyo raia wa Burkina Faso.

Simba ilitangulia kufanya mazungumzo na Aziz KI wakati huo akiwa na klabu yake ya ASEC na mazungumzo yote Mwanaspoti linafahamu kuwa yalikuwa yakifanyika chini ya usimamizi wa aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wao Barbara Gonzalez.

Ghafla Simba ikapunguza kasi kwenye mazungumzo hayo na Yanga ikachukua nafasi na kukimbiza mambo kwa haraka na kufanikiwa kumsainisha mkataba akienda kumaliza mwaka wa pili kwa mabingwa hao wa Tanzania.

Aziz KI sasa anaendelea kuipa mafanikio Yanga akiwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 15 na alikuwa kitovu cha mauaji yale ya Mnyama ya mabao 5-1 katika raundi ya awali ya ligi, ambapo alifunga bao moja na kupika jingine moja. Hadi sasa Aziz ameshaifunga mabao matatu Simba katika mechi tatu tofauti tangu aanze kuvaa jezi za njano na kijani.


MAXI MPIA NZENGELI

Kiungo Maxi Nzengeli anakaribia kuwa na msimu wake wa kwanza wa mafanikio katika soka la Tanzania akiwa na Yanga baada ya kuanza vizuri ndani ya timu yake hiyo akivizia taji lake la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu huu.

Awali, Maxi alikuwa akihitajiwa na Simba ambayo ilifanya maongezi naye ya awali, lakini baadaye Yanga tena ikajua kuhusu usajili huo na kuingilia kati kwenye dili na kumchukua. Maxi aliifunga Simba mabao mawili katika ile Kariakoo Dabi ya awali ya Ligi Kuu ambayo Mnyama alipasuka 5-1 na akawasha moto ile mbaya katika mechi ya mzunguko wa pili ambayo Yanga iliidunga SImba 2-1.

Katika ligi hadi sasa Maxi ana mabao tisa na asisti mbili.


JONAS MKUDE

Kiungo mkabaji wa Simba ambaye aliachwa mwisho wa msimu uliopita na Simba baada ya kuwa ameishi ndani ya klabu hiyo kwa takriban miaka 13, akatua Yanga na huu ni msimu wake wa kwanza.

Mkude amefufuka upya akiwa sehemu ya kikosi ambacho kimetengeneza ushindi mara mbili dhidi ya timu yake hiyo ya zamani iliyomkuza tangu akiwa kijana mdogo na kuanza kuchezea kikosi cha wakubwa msimu wa 2011-12.