Simba yatinga fainali Kombe la Muungano

Muktasari:

  • Mabao ya Simba yamefungwa na Freddy Michael dakika ya 25 na Israel Mwenda aliyehitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 90+4.

SIMBA imetinga fainali ya Kombe la Muungano baada ya leo kuichapa KVZ mabao 2-0 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mabao ya Simba yamefungwa na Freddy Michael dakika ya 25 na Israel Mwenda aliyehitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 90+4.

Simba inamsubiri mshindi wa mechi ya kesho Alhamisi kati ya Azam FC dhidi ya KMKM, ili kucheza naye fainali itakayopigwa Jumamosi Aprili 27, 2024 uwanjani hapo.

Michuano hiyo iliyosimama kwa takribani miaka 20, imerejea tena kwa kuanza kuzishirikisha timu nne pekee, Simba na Azam kutoka Tanzania Bara, huku KVZ na KMKM zikiiwakilisha Zanzibar. Hapo awali ilikuwa ikizishirikisha timu nane, nne za Tanzania Bara na zingine Zanzibar.

Rekodi za michuano hiyo zinaonyesha kwamba, Yanga SC ndiyo mabingwa wa kihistoria wakitwaa taji hilo mara nyingi (6) ikifuatiwa na Simba (5).

Baada ya leo kushuhudia nusu fainali ya kwanza, kesho itapigwa nusu fainali ya pili saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kati ya KMKM dhidi ya Azam.

Azam hii ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo, huku KMKM ni wakongwe wakiwa tayari wamebeba ubingwa mwaka 1984.

Bingwa wa michuano hiyo atakabidhiwa Sh50 milioni na mshindi wa pili kuondoka na Sh30 milioni