Suluhu na Yanga yaipa JKT mamilioni

Muktasari:

  • Kabla ya mchezo huo, mabosi wa JKT Tanzania waliwaahidi wachezaji wao kitita cha Sh60 milioni ikiwa ni sehemu ya motisha kama watapata ushindi dhidi ya vinara hao wa ligi huku Sh30 milioni ikipata sare.

MAAFANDE wa JKT Tanzania wamelamba Sh30 milioni baada ya kutoka suluhu (0-0) katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, jijini Dar es salaam.

Kabla ya mchezo huo, mabosi wa JKT Tanzania waliwaahidi wachezaji wao kitita cha Sh60 milioni ikiwa ni sehemu ya motisha kama watapata ushindi dhidi ya vinara hao wa ligi huku Sh30 milioni ikipata sare.

Mara baada ya mchezo huo, mmoja wa vigogo hao, Luteni Kanali Javan Bwai alienda katika vyumba vya kubadilishia nguo na kuwapongeza nyota hao kisha kuwapa utaratibu wa kupata mkwanja huo.

Kihesabu, kila mchezaji wa JKT Tanzania pamoja na benchi la ufundi na viongozi wengine wa timu hiyo watapata zaidi ya Sh500,000.

Matokeo ya mchezo wa leo,  yameifanya JKT Tanzania kupanda  kutoka nafasi ya 14 hadi 13 ikiwa na pointi 23 baada ya michezo 23, ikipambana kuepuka kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Timu hizo zilipokutana  mzunguko wa kwanza Agosti 29, 2023, JKT Tanzania ilichapwa mabao 5-0 na Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Baada ya suluhu hiyo, Yanga bado inaongoza msimamo ikiwa na pointi 59 baada ya michezo 23 na mchezo unaofuata itacheza na Coastal Union Aprili 27, huku JKT Tanzania ikicheza na Mtibwa Sugar Aprili 29.