Mabosi Liverpool wasimama katikati ya Slot na Salah

Muktasari:

  • Salah anadaiwa alichukizwa na kitendo cha kuanzishwa benchini katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 na alipoulizwa na waandishi juu ya kilichotokea baina yake na Klopp ambapo walirushiana maneno hadharani, alisema hawezi kuongea kwa sasa kwani akifanya hivyo moto utawaka.

LIVERPOOL, ENGLAND: Tangu straika wa Liverpool Mohamed Salah agombane na kocha wake Jurgen Klopp alipokuwa akifanyiwa mabadilko ya kuingia uwanjani katika mechi dhidi ya West Ham Jumamosi ya wiki iliyopita, kumekuwa na tetesi nyingi zinazomhusisha fundi huyo na kuondoka mwisho wa msimu huu kutua nchini Saudi Arabia.

Salah anadaiwa alichukizwa na kitendo cha kuanzishwa benchini katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 na alipoulizwa na waandishi juu ya kilichotokea baina yake na Klopp ambapo walirushiana maneno hadharani, alisema hawezi kuongea kwa sasa kwani akifanya hivyo moto utawaka.

Licha ya tetesi kudai kwamba Salah anataka kuondoka, kwanza kabisa mabosi wa Liverpool hawana mpango wa kumuuza kwa sasa na pia moja ya masharti yaliyowekwa na kocha Arne Slot anayedaiwa kuwa mbioni kutua Anfield, ni staa huyo wa Misri awepo katika timu.

Slot ambaye kwa sasa anaifundisha Feyenoord ameripotiwa kuwa ameshafanya makubaliano  na mabosi wa Liverpool kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo kwa msimu ujao kuchukua nafasi ya Jurgen Klopp ambaye ameshatangaza ataondoka mwisho wa msimu huu.

Salah amekuwa akiwindwa na timu za Saudi Arabia tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini alikataa ofa zao nono na kuamua kuendelea kusalia Liverpool.

Kwa sasa ameripotiwa kuwa hana furaha na mpango wake ni kuondoka kwenye kikosi cha majogoo hao wa Jiji la Liverpool mara baada ya msimu kumalizika.

Hata hivyo, bado ana mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika msimu ujao na hiyo inaonekana kuwa faida kwa Liverpool ambayo haitaki kuona staa huyo akiondoka.

Slot ni mmoja kati ya mashabiki wakubwa wa Salah na anaamini atafanya kazi vizuri zaidi staa huyo akiendelea kuwepo kwenye timu na ndio maana kaamua kuweka sharti la kuhitaji abakishwe.

Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana Al Ittihad ilimuwekea staa huyu wa kimataifa wa Misri mshahara unaofikia Pauni 2.4 milioni kwa wiki ikiwa ni ongezeko maradufu ukilinganisha na mkwanja wake anaoupokea kwa sasa ambao unafikia Pauni 1 milioni kwa wiki kwa mjumuisho wa bonasi mbali ya mshahara.

Staa huyu wa zamani wa Chelsea na AS Roma alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu mwaka 2022 na katika dirisha lililopita Liverpool ilikataa ofa ya Pauni 150 milioni kumuuza.

Hadi sasa inaaminika kuwa Ittihad haijakata tamaa kwenye mpango wa kuipata huduma ya staa huyu na inatazamiwa kumfuata tena.