Southgate amfungia vioo Jadon Sancho

Muktasari:

  • Ripoti hizo zinadai kwamba Sancho amechelewa sana kuonyesha ubora wake, hivyo kocha Southgate hawezi kufanya sapraizi yoyote kwenye uteuzi wa kikosi chake katika fainali hizo za Ujerumani.

LONDON, ENGLAND. Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya England, Gareth Southgate ameripotiwa kwamba hana mpango wa kumjumuisha fowadi wa Manchester United, Jadon Sancho kwenye kikosi chake kitakachokwenda kwenye michuano ya Euro 2024 huko Ujerumani wakati wa majira ya kiangazi.

Sancho amekuwa gumzo kwa sasa baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo timu yake anayochezea kwa mkopo kwa sasa Borussia Dortmund iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Paris Saint-Germain.

Tangu alipojiunga na Dortmund kwenye dirisha la Januari, kiwango cha Sancho kimekuwa kikiimarika kila siku na kuibua uvumi kwamba huenda kocha Southgate akamjumuisha kwenye kikosi cha Three Lions kwa ajili ya fainali hizo za Euro 2024, ambako wachezaji kwenye kikosi wameongezeka kutoka 23 hadi 26.

Hata hivyo, kwa mujibu wa The Mirror, licha ya kiwango matata cha Sancho, kocha Southgate hana mpango wa kumwita kwenye timu yake itakayokwenda kushindania ubingwa wa Ulaya.

Ripoti hizo zinadai kwamba Sancho amechelewa sana kuonyesha ubora wake, hivyo kocha Southgate hawezi kufanya sapraizi yoyote kwenye uteuzi wa kikosi chake katika fainali hizo za Ujerumani.

Bukayo Saka, Phil Foden, Jack Grealish, Jarrod Bowen, Marcus Rashford na Cole Palmer ni miongoni mwa wachezaji wanaomtangulia Sancho kwenye uteuzi wa kikosi hicho kwa wanaochezea pembeni.

Sancho hajaichezea England tangu 2021, ambapo kipindi chake kigumu alichopitia Man United kilimfanya kocha Southgate asimchague kwenye timu yake.

Sancho, 24, ni usajili wa pesa nyingi huko Man United aliponaswa akitokea Dortmund mwaka 2021, huku kwenye kikosi hicho cha Old Trafford amefunga mabao 12 na kuasisti sita katika mechi 82 alizocheza.

Sancho amerudi kwa mkopo Dortmund Januari mwaka huu baada ya kutibuana na kocha Erik ten Hag huko Man United. Na sasa Dortmund wanapiga hesabu za kumnyakua jumla mwisho wa msimu.

...