Ten Hag afunguka mipango yake

Muktasari:

  • Lakini, Mdachi huyo hatarajii kurudi kwao Uholanzi msimu ujao, akisema: "Nina hakika nitaendelea kuwa kocha wa Man United msimu ujao. Nimesaini mkataba mrefu hapa na mimi si mtu ninayezungumzia kuondoka."

MANCHESTER, ENGLAND. ERIK ten Hag anaamini ataendelea kuwa kocha wa Manchester United msimu ujao licha ya kuwapo kwa presha kubwa kuhusu usalama wa ajira yake kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

Mdachi huyo yupo kwenye hatari kubwa ya kupoteza kibarua chake wakati huu tajiri na mmiliki mpya wa miamba hiyo ya Old Trafford, Sir Jim Ratcliffe akipanga kuifumua na kuifuma upya timu hiyo.

Mwisho mbaya kwenye Ligi Kuu England msimu huu pamoja na kipigo kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City huenda ikafikisha mwisho ndoa ya Ten Hag na miamba hiyo ya Old Trafford.

Kocha huyo anahusishwa na mpango wa kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Ajax, ambayo ipo sokoni kusaka kocha mpya baada ya John van't Schip kubwaga manyanga.
Akizungumza na ViaPlay, Ten Hag hakutaka kufuta uwezekano wa kurejea kwenye klabu yake hiyo ya zamani.

Alisema: "Kuwasiliana na Ajax? Hapana. Huko baadaye, yeah kwanini isiwe? Ni klabu nzuri na nimekuwa na nyakati nzuri pale."

Lakini, Mdachi huyo hatarajii kurudi kwao Uholanzi msimu ujao, akisema: "Nina hakika nitaendelea kuwa kocha wa Man United msimu ujao. Nimesaini mkataba mrefu hapa na mimi si mtu ninayezungumzia kuondoka."

Ten Hag amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake Old Trafford - lakini tajiri Ratcliffe anaweza kumfuta kazi kabla hajamaliza miezi yake hiyo 12. Hilo linakuja baada ya miamba hiyo mabingwa mara 20 wa England kuhusishwa na mpango wa kumchukua kocha Thomas Tuchel atakapoondoka Bayern Munich.