Guede apeleka shangwe Yanga ikihitaji pointi 8 kutwaa ubingwa

Muktasari:

  • Bao pekee na la ushindi kwa Yanga limefungwa na nyota mshambuliaji wa timu hiyo, Joseph Guede katika dakika ya 41 baada ya kupiga shuti lililomshinda kipa wa Mashujaa, Patrick Munthar akiunganisha pasi ya Mudathir Yahya.

SHANGWE la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa Yanga msimu huu linaendelea kukaribia baada ya ushindi ilioupata wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa katika mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Bao pekee na la ushindi kwa Yanga limefungwa na nyota mshambuliaji wa timu hiyo, Joseph Guede katika dakika ya 41 baada ya kupiga shuti lililomshinda kipa wa Mashujaa, Patrick Munthar akiunganisha pasi ya Mudathir Yahya.

Guede aliyejiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Klabu ya Tuzlaspor ya Uturuki, ameendeleza kiwango bora akiwa na kikosi hicho kwani bao la leo ni la tano katika Ligi Kuu Bara.

Ushindi huu unaifanya Yanga kufikisha pointi 65 katika michezo 25 iliyocheza hivyo kuhitaji pointi nane tu ili kufikisha 73 zitakazowapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na ya 30 kwa ujumla kwani hazitaweza kufikiwa na timu yoyote.

Iko hivi, Azam FC inayoshika nafasi ya pili na pointi 54 hata ikishinda michezo yake yote sita iliyosalia itafikisha 72 huku kwa upande wa Simba iliyo ya tatu na pointi 50 ikishinda mechi zake zote saba itaishia na pointi 71.

Huu ni mchezo wa 13 kwa Yanga kucheza ugenini msimu huu katika Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo imeshinda tisa, sare miwili na kupoteza miwili pia ambapo imefunga mabao 24 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba na kukusanya pointi 29.

Mashujaa imeendeleza unyonge kwa Yanga kwani mechi ya mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex ilifungwa mabao 2-1, Februari 8, mwaka huu.

Mbali na hilo Mashujaa imeendelea kufanya vibaya kwani huu ni mchezo wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara bila kuonja ladha ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga JKT Tanzania bao 1-0 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Machi 6, mwaka huu.

Katika michezo 25 iliyocheza Mashujaa hadi sasa imeshinda mitano, sare minane na kupoteza 12 ikishika nafasi ya 14 na pointi 23.

Akizungumzia ushindi huo kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi aliwapongeza wachezaji wake kwa kupata pointi tatu licha ya wenyeji wao kuonyesha ushindani mkali kuanzia mwanzoni mwa mchezo huo kutokana na nafasi mbaya waliyopo.

"Tulitengeneza nafasi nyingi lakini tunashukuru tumeweza kutumia moja, kwangu nawapongeza wachezaji kwa kujitoa kwao na kuendelea kupigania hapa tulipo, ni furaha kwetu kuona tunaendelea kusimamia katika malengo tuliyojiwekea msimu huu," alisema Gamondi.

Kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed 'Baresi' amesema timu yake ilicheza vyema lakini ilizidiwa uzoefu ulioamua mechi hiyo, ambayo wenyeji walikaribia kupata bao la kusawazisha katika dakika za mwisho pale shuti la nyota wake lilipogonga besela na kutoka juu ya lango huku kipa wa Yanga, Djigui Diarra akiwa amevutika mbele.

Ushindi umemfanya Diarra kuboresha rekodi yake ya kutoruhusu mabao (clean sheet) kufikia 12 akimuacha mpinzani wake Ley Matampi wa Coastal Union mwenye nazo 10.