Kipa Msudani awadatisha mabosi Azam FC

Muktasari:

  • Azam FC ilimsajili kipa huyo kwa mkataba wa miezi sita kutoka klabu ya El Merreikh, mkataba ambao unamalizika mwisho wa msimu huu.

KIWANGO alichokionyesha kipa wa kimataifa wa Azam FC, Msudan Mohamed Mustafa, kimewashawishi viongozi wa klabu hiyo kuanza mchakato wa kukaa naye mezani kwa ajili ya mazungumzo ya mkataba mpya.

Azam FC ilimsajili kipa huyo kwa mkataba wa miezi sita kutoka klabu ya El Merreikh, mkataba ambao unamalizika mwisho wa msimu huu.

Alipoulizwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo ya Chamazi, Abdulkarim Amin 'Popat' kuhusiana na kipa huyo, alijibu wapo kwenye mchakato wa kumuongezea mkataba mpya kutokana na kiwango alichokionyesha tangu ajiunge nao.  

"Tutamuongezea mkataba mpya, amekuwa na msaada mkubwa kwa timu, hivyo tumeanza mchakato kwa kuzingatia kanuni na sheria zinavyotaka.

Aliongeza: "Soka linachezwa sehemu za wazi na ndio maana kocha amekuwa akimtumia mara kwa mara kikosini, angekuwa hana msaada sidhani kama angekuwa anapangwa, ndio maana kama vingozi tumeona umuhimu wa kuendelea naye msimu ujao."

Aliyekuwa beki wa kati wa timu hiyo, Agrey Morris alisema kipa Mustafa ameongeza nguvu katika safu ya ulinzi. "Ni kipa mzuri, naamini viongozi wataona haja ya kuendelea naye, sina maana waliopo wengine ni wabaya, ila inatakiwa awepo ambaye ni tegemeo wa kikosi cha kwanza."