Rekodi tatu Yanga ikiukaribia ubingwa

Muktasari:

  • Rekodi ya kwanza ambayo Yanga imeweka kutokana na bao la Mudathiri Yahya dakika ya 83 katika mchezo huo ni kuwa timu pekee msimu huu wa 2023/24 iliyoshinda dhidi ya wapinzani wote 15 wanazoshiriki Ligi Kuu Bara.

USHINDI wa bao 1-0 ambao Yanga iliupata juzi Jumatano dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, ulikifanya kikosi hicho cha Miguel Gamondi kuweka rekodi tatu tofauti huku wakiendelea kuunyemelea ubingwa wa 30 wa Ligi Kuu Bara.

Rekodi ya kwanza ambayo Yanga imeweka kutokana na bao la Mudathiri Yahya dakika ya 83 katika mchezo huo ni kuwa timu pekee msimu huu wa 2023/24 iliyoshinda dhidi ya wapinzani wote 15 wanazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Kagera Sugar inayonolewa na Fred Felix Minziro ndio timu pekee ambayo ilikuwa imeiwekea ngumu Yanga kutokana na mchezo wa kwanza kule Kagera kwenye Uwanja wa Kaitaba kumalizika kwa suluhu hivyo Gamondi na vijana wake ilibidi kutumia nguvu ya ziada Chamazi ili kuweka rekodi hiyo.

Rekodi nyingine ambayo Yanga imeweka ni kushinda michezo 25 mfululizo katika ligi tangu msimu uliopita, mara ya mwisho kwa Wananchi kudondosha pointi nyumbani ilikuwa Oktoba 23, 2022 ambapo walitoka sare ya bao 1-1 dhidi wa watani zao Simba.

Kwa hesabu za msimu huu wa 2023/24, Yanga ina rekodi ya ushindi kwa asilimia 100 ikiwa nyumbani kuliko timu nyingine yoyote, wameshinda mechi zao zote 13, wanaowafuatia ni Azam FC ambao katika michezo 13, wameshinda 10, sare mbili na kupoteza mara moja.

Watani wao Simba wenyewe wanashika nafasi ya tatu katika michezo 12 wameshinda mara nane sare mbili na kupoteza mara mbili.

Rekodi ya tatu ambayo Yanga iliweka baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kagera Sugar ni kufikisha michezo mitano mfululizo katika mashindano yote kucheza bila ya kuruhusu bao. Michezo hiyo ni dhidi ya JKT Tanzania (0-0), Coastal Union (1-0), Tabora United (3-0), Mashujaa (1-0) na Kagera Sugar (1-0).

Katika michezo 10 iliyopita ya mashindano yote ikiwemo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, Yanga imeruhusu bao moja tu ambalo ni dhidi ya Simba walilofungwa na Freddy Michael wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika ligi.

MSIKIE GAMONDI

Licha ya ugumu wa michezo ambayo wamekumbana nayo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye alionekana katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar akigeuka mbogo kwa mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu, amewapongeza wachezaji wake kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitoa kuhakikisha wanafanya vizuri.

"Japo yapo matukio ambayo yamekuwa yakituumiza lakini lazima tukubali kwamba wachezaji wangu wamekuwa wakifanya kazi kubwa, tunatakiwa kuendelea na mapambano bila ya kuchoka na kuangali vikwazo vilivyopo," alisema kocha huyo na kuongeza;

"Tupo hatua chache nyuma kufanikisha kile ambacho tunakihitaji."

Kabla ya mchezo wa jana kati ya Azam FC dhidi ya Simba, Yanga ilikuwa ikihitaji pointi tano tu kutawazwa kuchukua ubingwa wa 30 ligi kuu.

Timu hiyo ina michezo minne iliyobaki kumaliza msimu huu katika ligi ambayo miwili ni ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji huku ikimalizia msimu nyumbani kwa kukabiliana dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons.

REKODI ZILIVYO

Tangu mara ya mwisho Yanga kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Simba Oktoba 23, 2022, baada ya hapo msimu wa 2022/23 ilicheza mechi 12 mfululizo nyumbani na kushinda zote huku ikifunga mabao 30 na kuruhusu manne, clean sheet tisa.

Matokeo ya mechi hizo 12 ni; Yanga 1-0 KMC, Yanga 4-1 Singida Big Stars, Yanga 2-0 Mbeya City, Yanga 1-0 Prisons, Yanga 3-0 Polisi Tanzania, Yanga 3-0 Coastal Union, Yanga 1-0 Ihefu, Yanga 1-0 Ruvu Shooting, Yanga 2-0 Namungo, Yanga 3-1 Geita Gold, Yanga 5-0 Kagera Sugar na Yanga 4-2 Dodoma Jiji.

Kwa msimu huu katika mechi 13 za nyumbani ambazo Yanga imeshinda zote, imefunga mabao 33 na kuruhusu matano wakati clean sheet zikikusanywa tisa.

Kwa upande wa matokeo ya mechi hizo 13 ni; Yanga 5-0 KMC, Yanga 5-0 JKT Tanzania, Yanga 1-0 Namungo, Yanga 3-2 Azam, Yanga 2-0 Singida Fountain Gate, Yanga 4-1 Mtibwa Sugar, Yanga 1-0 Dodoma Jiji, Yanga 2-1 Mashujaa, Yanga 5-0 Ihefu, Yanga 1-0 Geita Gold, Yanga 2-1 Simba, Yanga 1-0 Coastal Union na Yanga 1-0 Kagera Sugar.

Nyota wa zamani wa Tukuyu Stars na Coastal Union, Charles Makwaza ambaye kwa sasa ni mchambuzi, alisema Yanga imekuwa bora kila eneo na matokeo yake si ya kushangaza.

Beki huyo alisema kwa mwenendo ilionao ni wazi inaweza kutangaza ubingwa mapema hata kabla ya michezo yake kuisha, akieleza kuwa maandalizi na mipango imara ya utawala ndio siri kubwa.

“Yanga kila mchezaji amekuwa staa, hii ni kutokana na mipango ya uongozi nafikiri matokeo hayo hakuna wasiwasi kwamba wanaweza kumaliza shughuli kabla ligi kuisha” alisema Beki huyo.