Bunduki sita za kuifaa Arsenal

Muktasari:

  • Straika huyo wa Kocha Mikel Arteta amepoteza nafasi na sasa anawekwa benchi na nafasi yake kupangwa Kai Havertz baada ya Mbrazili huyo kufunga mabao manne tu katika mechi 24 alizocheza kwenye ligi.

LONDON, ENGLAND: Arsenal huenda ikaingia sokoni kusaka straika mpya kabla ya kuanza kwa msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu England baada ya Gabriel Jesus kiwango chake kushuka na haijulikani kama ataendelea kuwapo Emirates.

Straika huyo wa Kocha Mikel Arteta amepoteza nafasi na sasa anawekwa benchi na nafasi yake kupangwa Kai Havertz baada ya Mbrazili huyo kufunga mabao manne tu katika mechi 24 alizocheza kwenye ligi.

Kinachoelezwa, kiwango kibovu kwenye kupasia mipira kwenye nyavu pamoja na majeruhi mfululizo yanaonekana kuwa tatizo kwa mshambuliaji huyo kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho hadi msimu ujao.

Hata hivyo, huko sokoni kuna idadi ndogo ya washambuliaji Namba 9 wenye uwezo wa kufunga mabao, hivyo, Arsenal italazimika kutumia pesa nyingi katika kupata mshambuliaji mpya.

Hii hapa ni orodha ya mastraika sita ambao Arsenal inaweza kwenda kunasa mmoja na kumaliza tatizo lao la kuwa na straika anayefunga mabao kuleta mambo matamu kwenye kikosi cha kocha Arteta.

1.Alexander Isak;

Straika huyo wa Newcastle United anaweza kuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Arteta kwa msimu wa 2024/25. Kitu kizuri kwao ni Newcastle ipo tayari kumuuza ili kupata pesa ambazo zitawafanya kwenda na masharti ya mapato na matumizi kwenye kikosi chao. Isak ni moja ya wachezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha St James’ Park pamoja na kiungo Bruno Guimaraes. Isak amefunga zaidi ya mabao 20 kwenye michuano yote msimu huu na yupo kwenye mbio za kusaka Kiatu cha Dhahabu msimu huu.

2.Victor Osimhen;

Mwaka jana alikuwa tishio sana na ubora wake kwenye kutikisa nyavu uliisaidia Napoli kunyakua taji la Serie A msimu uliopita. Straika huyo wa Napoli, kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka kwenye kikosi hicho, ambapo alifunga mabao 26 katika mechi 32 za ligi za msimu uliopita. Msimu huu ameshuka kidogo, lakini bado amefanikiwa kufunga mabao 14 ya ligi.

3.Viktor Gyokeres;

Straika huyo wa Sporting CP ni kama Osimhen, kuna matarajio makubwa ya kubadili timu kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Bila shaka ushindani wa kunasa saini yake utakuwa mkubwa, hivyo Arsenal wanapaswa kufanya haraka kama kweli wapo na dhamira ya dhati ya kumsajili mshambuliaji huyo wa Sporting CP. Timu nyingi zinamhitaji staa huyo, ambaye amefunga mabao 40 katika michuano yote na bado msimu haujamalizika.

4.Benjamin Sesko;

Kama Arsenal inahitaji mshambuliaji wa kumtumia miaka mingi, basi wanaweza kuchangamkia huduma ya mkali wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, ambaye amekuwa kwenye rada za klabu kibao kubwa za Ulaya zikihitaji saini yake. Fowadi huyo wa kimataifa wa Slovenia anafanya vizuri na katika msimu wake wa kwanza kwenye Bundesliga, amefunga mabao 11 katika mechi 30. Sesko umri wake ndiyo kwanza miaka 20, hivyo Arsenal itakuwa na huduma yake kwa muda mrefu itakapomnasa.

5.Ivan Toney;

Kwa muda sasa huduma ya straika huyo wa Brentford imekuwa ikihusishwa na Arsenal. Hata hivyo, straika Ivan Toney yupo pia kwenye rada za timu nyingine jambo linalowapa jeuri klabu yake ya Brentford kumuuza kwa bei kubwa mshambuliaji hiyo. Lakini, kama Arsenal itakuwa siriazi na kuweka ofa mezani bila ya shaka Toney atalazimisha uhamisho huo kutokea. Nguvu ndiyo silaha ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, hivyo bado kuna kitu anachoweza kukifanya uwanjani kwa muda mrefu.

6.Dominic Solanke;

Kama Arsenal itakosa huduma ya Toney, mshambuliaji anayefanana na mkali huyo ni yule straika wa Bournemouth, Dominic Solanke. Kinda huyo wa zamani wa Chelsea, aliyewahi pia kukipiga Liverpool ameonyesha kiwango kikubwa sana msimu huu, akichuana kwenye mbio za kufukuzia Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England sambamba na wakali kama Erling Haaland, Isak na Ollie Watkins. Solanke uwezo wake wa kufunga ni mkubwa kuliko wa Jesus, hivyo Arsenal ikifanikiwa kumnasa itakuwa imepiga hatua kubwa katika kumaliza tatizo lao la kuwa na mabao kwenye idara yao ya ushambuliaji.