Pep aipa Arsenal ubingwa

Muktasari:

"Kwanza hatuwapati kwenye utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa na namna wanavyocheza kila siku wanazidi kuwa bora na wanacheza kwa kiwango kilekile, zimebaki mechi tatu..." - Pep

KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amesisitiza kwamba Arsenal ina nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu ikiwa wao wataangusha pointi katika mechi moja kati ya tatu zilizosalia.

Man City ambayo haijafungwa kwenye mechi 20 mfululizo iliendeleza rekodi hiyo jana Jumamosi baada ya kushinda mabao 5-1 dhidi ya Wolves ambapo staa wao Erling Haaland alifunga manne.

Kwa sasa vijana hao wa Guardiola wapo nafasi ya pili nyuma ya Arsenal wanaoongoza kwa pointi zao 83 ikiwa ni tofauti ya pointi moja dhidi yao lakini Man City ina faida ya kuwa na mchezo mmoja mkononi.

"Jambo zuri zaidi kwetu ni kwamba kuna wiki mbili zimesalia kabla ya ligi kumalizika lakini sisi tuna mechi tatu ambazo tukishinda zote na kuchukua alama tisa basi tutakuwa mabingwa lakini kama tutashindwa kukusanya pointi zote labda tukapata saba au chini ya hapo basi naona kabisa Arsenal itakuwa bingwa," alisema Guardiola na kuongeza.

"Kwanza hatuwapati kwenye utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa na namna wanavyocheza kila siku wanazidi kuwa bora na wanacheza kwa kiwango kilekile, zimebaki mechi tatu ni matumaini yangu tutashinda mechi ya kwanza, ya pili na ya tatu, hatma ya kuchukua ubingwa ipo mikononi mwetu.

"Unaona matokeo ya 5-1 tuliyopata ni mazuri lakini sijaridhishwa na namna tulivyocheza, tulipoteza mipira mingi kirahisi."

Katika mechi tatu zilizosalia Man City itacheza dhidi ya Fulham, Tottenham na West Ham wakati Arsenal mbili zilizosalia itakutana na Man United na Everton.