Saraphina, Zuchu, Nandy shida yao iko hapa

Muktasari:

  • Wawili hao kutoonekana wakiwa pamoja ilizua gumzo na minong’ono kuwa huenda ni kuna uhusiano mbaya kati yao. Saraphina amelijibu hilo, akisema:

RHOBI CHACHA

UKIAMBIWA kutaja wasanii wa kike wanaofanya vizuri Bongo Fleva na wenye sauti tamu masikioni mwa watu wakiwa wanaimba basi hutaacha kumgusia Saraphina Michael ‘Phina’ binti wa ngoma ya ‘upo nyonyo upo titi’.

Phina amekuwa akihusishwa sana na baadhi ya mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva kuwa ana bifu na wasanii wenzake wa kike wenye sauti tamu kama yake ambao ni Zuchu, Nandy na Ruby, lakini yeye mwenyewe amefafanua hilo kwenye mahojiano na Mwanaspoti.

Kama itakumbukwa, Saraphina ni zao la shindano la kusaka vipaji Bongo Star Search ‘BSS’ mwaka 2018. Katika mahojiano hayo, ameliambia Mwanaspoti kuwa, hana bifu na wanamuziki hao waliotajwa ila tu baadhi ya mashabiki ndio wanaotaka awe na bifu na hao wanamuziki.

“Mie nasema si Zuchu, wala Nandy na hata huyo Ruby mimi sina bifu naye na wala siwezi kabisa, ila naona ni mashabiki ndio wanaotamani mimi niwe na bifu nao hadi na hao baadhi ya hao wanamuziki nimewaona kama wanafuata maneno ya mashabiki.

“Sitaki kumtaja au kuwataja kati ya hao wanamuziki wa kike nilioambiwa nina bifu nao kuwa wananifanyia bifu mimi na hii naona kabisa wanafuata maneno ya mashabiki wanayoyazusha ili iwe kweli sasa mimi najiuliza kwamba, wanapenda ili kupromoti kazi zao au wanapenda ili mradi tu wazungumziwe?

“Sijapata jibu sababu hata nikikutana nao kuna baadhi ya vitu naviona haviko sawa kati ya hao ila mimi kiukweli sina bifu kabisa nao,” anasema Phina.

MSOME HAPA

Saraphina aliingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za Soundcity MvP 2023 huko Nigeria. Wasanii wa kike kutoka Tanzania waliotajwa  kuwania tuzo za Soundcity MVP kwa mwaka 2023 ni pamoja na Phina ambaye aliiteka Tanzania mwaka 2022 na ngoma yake ya ‘Upo Nyonyo’ alitajwa kuwania kipengele cha Msanii bora Chipukizi huku Zuchu alitajwa kuwania tuzo hizo pia ambapo aliwania kipengele cha Msanii Bora Mwaka, Msanii Bora Wa Kike, Video Bora ya Mwaka na Msanii Bora.

Phina anasema tuzo hizo ndio kitu kilichozua gumzo kwa baadhi ya mashabiki kuwa wako sehemu moja na Zuchu lakini hakuna picha iliyoonyesha Saraphina akiwa na mwimbaji huyo nyota wa WCB, Zuchu, ambaye pia alikuwa Nigeria kwa ajili ya tuzo hizo.

Wawili hao kutoonekana wakiwa pamoja ilizua gumzo na minong’ono kuwa huenda ni kuna uhusiano mbaya kati yao. Saraphina amelijibu hilo, akisema:

“Kwanza, huenda tulionana lakini hatukupiga picha. Pili, nilichelewa kufika (Nigeria). Nilipofika, nilienda moja kwa moja kufanya majaribio ya steji kwa ajili ya shoo. Baada ya hapo, nilienda hotelini.”

Kwa upande mwingine, Saraphina alimzungumzia mkali mwingine wa muziki, Rubby, akisema anashangaa kusikia kuna bifu kati yao.

“Sijawahi kugombana na Rubby. Ninachojua ni kwamba ilitokea kutokuelewana kidogo tu kati ya uongozi wangu na Ruby na sio mimi na Ruby.

“Wakati tukiwa lokesheni kurekodi wimbo wangu wa ‘Namba One’, kuna vitu Ruby alikuwa anahitaji. Baadaye alipatiwa na tukaendelea na kazi na nyimbo inafanya vizuri,” anasema.

Tangu hapo, Saraphina hajawahi kurudi nyuma. Baadhi ya ngoma zake zinazoendelea kufanya vizuri sokoni ni ‘Upo Nyonyo’, ‘Smile’, ‘Raha’ na ‘Zinduna’ aliyoiachia hivi karibuni.

KUIGIZA MAISHA

Kwa muda mrefu, yamekuwapo madai kuwa Saraphina amekuwa akiishi maisha ya juu tofauti na uhalisia ili tu aonekane ni msanii mkubwa.

“Sijui haya mambo yanatoka wapi. Ninachofahamu ninaishi maisha ninayoyamudu. Kila ninachofanya kipo ndani ya uwezo wangu. Ukweli ni kwamba siwezi kujiumiza ili nionekane nipo juu, kwani nilishajifunza kwa wasanii maarufu walionitangulia” anasema.

KUMBE HAVAI KIGODORO

Kuna kipindi kulizuka mitandaoni kwa madai ya kuwa Phina shepu yake ni feki yaani kigodoro kama wanavyoeleza mitandaoni.

“Nilijua lazima hili swali niulizwe lakini kiukweli sijawahi kuvaa kigodoro nina shukuru Mungu ameniumba nikaumbika ukizingatia mimi ni mtoto wa Kisukuma sifa zetu zinajulikana  hivyo sijawahi kufikiria kufanya upasuaji wa aina yoyote wala kuvaa kigodoro ili niwe na muonekano kwani mimi nimeridhika ana nilivyoumbwa na Mungu.”

Phina ambaye anatamba hadi sasa na nyimbo kama ‘Sio Kitoto’ ‘Sitaki Tena’, ‘Kushki’, ‘Pekecha’, ‘Wamerudiana’ na ‘Upo Nyonyo’ na nyingine nyingi anasema aliweka mapenzi pembeni ili afanye muziki anasema aliweka mapenzi pembeni ili afanye muziki lakini kwasasa yuko tayari kuingia kwenye uhusiano ila anahitaji mwanaume ambaye anafahamu kuwa kazi yake ni ya muziki na hawezi kuiacha.