Championship ilikuwa ni msimu wa jasho na damu

Muktasari:

  • Wakati ligi hiyo ikitamatika yapo mambo mengi yaliyojitokeza tangu msimu huu ulivyoanza kama ambavyo Mwanaspoti linavyokudadavulia chini.

MSIMU uliopita wa Ligi ya Championship ulifika tamati mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kivumbi, jasho na damu kuvuja kwa wachezaji wa timu 16 zilizokuwa zinapigania nafasi mbalimbali hususan lengo kuu la kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Wakati ligi hiyo ikitamatika yapo mambo mengi yaliyojitokeza tangu msimu huu ulivyoanza kama ambavyo Mwanaspoti linavyokudadavulia chini.


KENGOLD, PAMBA ZAWEKA REKODI

KenGold ilikuwa ni timu ya kwanza msimu huu kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi baada ya kuonyesha soka safi tangu mwanzoni kufuatia kusota katika ligi hiyo kwa takribani misimu mitatu hadi ilipotimiza lengo.

Timu hiyo ya Mbeya imekuwa mabingwa baada ya kukusanya pointi 70 ikifuatiwa na Pamba iliyomaliza ya pili na pointi 67 huku ikipanda Ligi Kuu Bara msimu ujao kwa rekodi ya kipekee kufuatia kusota takribani miaka 23 tangu iliposhuka 2001.

MBEYA KWANZA, BIASHARA VITA NZITO

Wakati timu mbili zilizomaliza nafasi ya kwanza na pili zikipanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja, vita kwa sasa imebaki kwa Mbeya Kwanza iliyomaliza ya tatu na pointi 65 na Biashara United iliyoshika ya nne baada ya kukusanya pointi zake 62.

Timu hizi zitakutana katika mchezo wa ‘Play-Off’ (mtoano) ambapo mechi ya kwanza itapigwa Juni 4 na marudiano yakipigwa Juni 8 na mshindi wa jumla atakutana na atakayepoteza kutoka Ligi Kuu Bara kwa atakayemaliza kwenye nafasi ya 13 na 14.

Mchezo huu ni wa kiasi kwani timu hizi zilishuka pamoja Championship msimu wa 2021/2022 ambapo Biashara United ilimaliza na pointi 28 baada ya kushinda michezo mitano, sare 13 na kupoteza 12 ikimaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo msimu huo.

Kwa upande wa Mbeya Kwanza iliburuza mkia na pointi 25 msimu huo baada ya kushinda michezo mitano, sare 10 na kupoteza 15.

Mchezo wa kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huo kwa timu hizo kukutana ulipigwa Oktoba 29, 2021 ambapo zilitoka sare ya bao 1-1 huku mechi ya marudiano iliyochezwa Uwanja wa Musoma Mara, Biashara United ilishinda bao 1-0, Aprili 6, 2022.


RUVU, PAN KUSHIRIKI FIRST LEAGUE

Ruvu Shooting iliyoshuka daraja msimu uliopita, imeendelea kujikuta ikishuka zaidi kwani msimu ujao itashiriki Ligi Daraja la Pili (First League) baada ya kuburuza mkiani na pointi 13 kufuatia kushinda michezo miwili kati ya 30.

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara 1982, Pan Africans ya jijini Dar es Salaam ambayo ilitwaa pia taji la Muungano imeungana na Ruvu kushuka moja kwa moja baada ya kumaliza nafasi ya 15 kufuatia kushinda michezo mitano, sare tano na kupoteza 20.


KAZI IPO HUKU

Michezo mingine ya mtoano itakayovuta hisia za mashabiki ni ile itakayozikutanisha timu zilizomaliza nafasi ya 11, 12, 13 na 14 kusaka tiketi ya kubaki msimu ujao kwenye ligi hiyo wakati zitakapopambana zenyewe kisha kukutana na za First League.

Stand United iliyomaliza ya 11 na pointi 32 itacheza na Green Warriors iliyoshika ya 12 na pointi 31 huku Transit Camp iliyohitimisha msimu ya 13 na pointi zake 27 itapambana na kikosi cha Kocha Feisal Hau, Copco FC kilichomaliza ya 14 na pointi 25.

Timu mbili zitakazoshinda zitasalia katika Ligi ya Championship msimu ujao na nyingine mbili zitakazopoteza zitakuwa na kibarua kingine cha kujitetea wakati zitakapocheza tena mechi za mtoano na za First League kusaka tiketi ya kupanda.


NYOTA KENGOLD AWEKA REKODI

Mshambuliaji wa KenGold, Edgar William ameweka rekodi mpya katika ligi hiyo baada ya kufikisha jumla ya mabao 21 msimu huu hivyo kumpita mchezaji na mfungaji bora msimu uliopita nyota wa JKT Tanzania, Edward Songo aliyemaliza kinara na 18.

Songo aliyeiwezesha timu hiyo kupanda Ligi Kuu Bara msimu huu alimaliza kinara kwa misimu miwili mfululizo akianza na 2021/2022 alipofunga mabao 16 na 2022/2023 akimaliza na 18 huku yote akiyafunga na kikosi cha Maafande wa JKT Tanzania.


HAT-TRICK (5)

Msimu huu zimefungwa jumla ya ‘Hat-Trick’ tano ambapo nyota waliofunga ni Kika Salum (Pan Africans), wakati ilipoifunga Copco mabao 3-2 (Septemba 9, 2023), Abdulaziz Shahame (TMA FC) iliposhinda 6-1 dhidi ya Stand United (Januari 6, 2024).

Wengine ni Oscar Mwajanga wa Mbeya Kwanza aliyefunga wakati wakishinda mabao 4-1 dhidi ya Ruvu Shooting (Februari 4, 2024) na Boban Zirintusa wa Biashara United aliyefunga mbili akianza na 3-0, mbele ya Ruvu Shooting, (Novemba 11, 2023).

Boban alifunga pia ‘hat-trick’ ya pili msimu huu wakati timu hiyo ilipoifunga Pan Africans mabao 4-0 mechi iliyopigwa Desemba 11, 2023 na kuhitimisha ya tano ikiwa ni nyingi tofauti na msimu uliopita wa 2022/2023 zilipofungwa tatu tu.


KIPA AFUNGA BAO

Kipa wa Biashara United, David Kissu Mapigano aliweka rekodi ya makipa wa Championship waliofunga bao wakati timu hiyo iliposhinda mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliopigwa Februari 15, 2024 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Musoma mkoani Mara.

Bao lingine katika mchezo huo lilifungwa na Abeid Athuman likiwa ni la kwanza kwa nyota huyo akiwa na kikosi hicho tangu aliposajiliwa kwenye dirisha dogo la Januari 2024, baada ya kuachana na timu ya Geita Gold inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Mara ya mwisho kwa kipa wa Championship kufunga bao alikuwa ni Mkongomani, Alain Ngeleka aliyekuwa anaichezea Kitayosce kwa sasa Tabora United aliyefunga licha ya kupoteza mabao 3-1, dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Desemba 3, 2022.

Kissu alijiunga na Biashara United msimu uliopita akitokea Klabu ya KMC huku akiwahi kuchezea timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi zikiwemo, Simba, Azam FC, Namungo, Singida United, Toto Africans za Tanzania na Gor Mahia ya kwao Kenya.


WASIKIE WADAU

Kocha Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu huu anasema haikuwa rahisi kutokana na ushindani uliokuwa unaonyeshwa na kila klabu hasa unapokwenda kucheza michezo ya ugenini kwa sababu huwa migumu zaidi.

“Wadhamini waliongeza ushindani sana kwa sababu hata yale matukio ya ajabu ambayo tumeyazoea kuyaona msimu huu kwa kiasi kikubwa hayakuwepo, hii ni ligi bora sana hapa nchini na kama wawekezaji watazidi kujitokeza ushindani utakuwa mkubwa,” anasema Challe.

Kocha Mkuu wa Biashara United, Amani Josiah anasema umekuwa msimu bora kutokana na ushindani mkubwa ulioonyeshwa na kila timu huku akiweka wazi licha ya kutopanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja ila wanajipanga na mtoano.