Guede ni habari nyingine Yanga, awapiga bao Mzize, Musonda

Muktasari:

  • Awali Guede alionekana kuwa na mwanzo mgumu katika kikosi cha kocha Miguel Gamondi lakini kadiri muda ulivyokuwa ukisogea ameonekana kubadili upepo wa mambo huko Jangwani kiasi cha kuwazidi kete, Clement Mzize na Kennedy Musonda ambao amekuwa akigombania nao namba na hata viungo wa timu hiyo.

Ni kama gari limewaka zaidi kwa mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede ambaye hivi sasa namba zake zinambeba na kumfanya kuwa mchezaji hatari  kwenye kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na Kocha Miguel Gamondi.

Awali Guede alionekana kuwa na mwanzo mgumu katika kikosi cha kocha Miguel Gamondi lakini kadiri muda ulivyokuwa ukisogea ameonekana kubadili upepo wa mambo huko Jangwani kiasi cha kuwazidi kete, Clement Mzize na Kennedy Musonda ambao amekuwa akigombania nao namba na hata viungo wa timu hiyo.

Fowadi huyo ambaye alijiunga na Yanga wakati wa dirisha dogo la usajili msimu huu baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu tangu alipoachana na Tuzlaspor ya Uturuki, amehusika katika mabao sita kwa kufunga matano na kutoa asisti moja  ndani ya michezo sita iliyopita ya mashindano yote kwa maana nyingine ana wastani wa kuhusika na bao katika kila mchezo.

Katika michezo hiyo sita iliyopita kwa Yanga katika mashindano yote, Guede mwenye miaka 29 namba zake ni kubwa kuliko hata Stephane Aziz KI ambaye amekuwa akiimbwa kwenye kikosi hicho akiwa na mabao 15 katika ligi.

Guede hajafunga katika mchezo mmoja tu kati ya hiyo sita dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania ambao ulimalizika kwa suluhu, balaa lake lilianza dhidi ya Singida Fountain Gate alipofunga mabao mawili wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0, akafunga tena bao moja dhidi ya Simba.

Baada ya kuzuiwa katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania, moto wake uliendelea dhidi ya Coastal Union bao lake liliifanya Yanga kuendelea kuusogelea ubingwa wa ligi, kituo kilichofuata kilikuwa jana Jumatano dhidi ya Tabora United ambapo bao lake liliisaidia Yanga kushinda 3-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Kwa sasa Guede ndiye mchezaji mwenye wastani mzuri na mkubwa katika kuhusika katika mabao ya Yanga ndani ya michezo sita iliyopita huku akifuatiwa na Aziz Ki mwenye mabao matatu, Kennedy Musonda (1) huku Mzize akiwa hajafunga bao lolote licha ya kuwa kinara wa mabao kwenye Kombe la FA akifunga matano.

Pamoja na kwamba hakuanza msimu akiwa na Yanga, Guede katika Ligi Kuu Tanzania Bara amemfikia kwa mabao Mzize mwenye manne na kumpita Musonda mwenye matatu huku akitumia dakika 746 katika mechi 12 tu. Mzize ametumia dakika 1113 katika mechi 23, Musonda dakika 875 katika mechi 19.

Akizungumzia mwenendo wake, Guede amesema: "Nina furaha kuisaidia timu yangu kupata matokeo, naamini nina nafasi ya kuendelea kufanya zaidi kadiri ya vile ambavyo ninapata nafasi kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu."

Kwa sasa Guede ndiye mshambuliaji kiongozi kwenye safu ya Yanga ambayo mara kadhaa Gamondi amekuwa akifanya mabadiliko ili kutoa nafasi kwa kila mchezaji kulingana na mipango ya kila mchezo ambao ulikuwa mbele yao.