Israel Mwenda apewa miwili Simba, mwenyewe afunguka

Muktasari:

  • Mwanaspoti linafahamu kuwa takribani wachezaji watano wa Simba mikataba yao inatamatika mwishoni mwa msimu huu akiwemo Kibu Denis, Sadio Kanoute na Kennedy Juma.

Kwa sasa mashabiki wa Simba wako njia panda juu ya timu yao hususani ishu ya usajili, lakini taarifa njema ni kwamba mlinzi wa kulia, Israel Mwenda ameongeza mkataba mpya kuendelea kukipiga kikosini hapo.

Mwanaspoti linafahamu kuwa takribani wachezaji watano wa Simba mikataba yao inatamatika mwishoni mwa msimu huu akiwemo Kibu Denis, Sadio Kanoute na Kennedy Juma.

Inaelezwa kuwa Simba imefikia uamuzi wa kumuongezea Mwenda mkataba wa miaka miwili hadi 2025 ili kuongeza ushindani eneo la beki wa kulia ambalo Shomari Kapombe amekuwa akifanya vizuri.

"Kapombe amekuwa akicheza hapo na anakosa mapumziko, kama binadamu kuna muda anachoka kwa kucheza mechi mara kwa mara bila kupumzika hivyo tukaona tumuongezee mkataba Mwenda," alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili Simba (jina tunalo) na kuongeza.

"Licha ya hivyo pia Kapombe hayuko sawa na Mwenda amecheza mechi tatu za ligi na kuwashawishi viongozi kwa kiwango chake, ataendelea kuwepo kikosini."

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenda alisema; "Ni kweli mkataba wangu unaisha lakini bado sijazungumza na viongozi wangu, ishu ya usajili wala haijifichi ikitokea mtasikia tu."

Hivi karibuni Mwenda amekuwa akipata nafasi ya kucheza kutokana na Kapombe kupata majeraha kwenye mechi dhidi ya Ihefu, Aprili 13, mwaka huu Simba ikitoka sare ya  bao 1-1.

Mwenda alicheza dakika 90 dhidi ya Yanga, Simba ilipopoteza kwa mabao 2-1, Namungo 2-2 na Mashujaa 1-1 kwenye mashindano ya Kombe la FA ambapo Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 6-5. Pia akacheza mechi za Kombe la Muungano dhidi ya KVZ na Azam FC.