Mziki wa Mzize wakamata makocha

Muktasari:

  • Mzize licha ya kuandamwa na mashabiki wa Yanga, lakini sokoni amekuwa akiwachanganya makocha wengi akiwa tayari na ofa ya Azam iliyotenga dau la kufuru kumnunua mshambuliaji huyo kutokea Yanga.

Mashabiki majukwaani wanalia na mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize lakini upande wa pili kwa makocha wanamwona mshambuliaji huyo kuwa ni bidhaa adimu kisha wakafunguka juu ya vitu vinavyompa thamani na kumuangusha.

Mzize licha ya kuandamwa na mashabiki wa Yanga, lakini sokoni amekuwa akiwachanganya makocha wengi akiwa tayari na ofa ya Azam iliyotenga dau la kufuru kumnunua mshambuliaji huyo kutokea Yanga.

Mbali na ofa hiyo ya Azam mapema Mzize aliwahi kuhitajiwa na klabu ya Olympic De Marseille ya Ufaransa lakini inatajwa pia klabu ya Watford ya England kumuwania mshambuliaji huyo.

Hata makocha mbalimbali wamefungukia ubora wake wa kwanza akiwa kocha wa Far Rabat ya Morocco, Nasredine Nabi, akisema hakuna kocha atakayefanya kazi na Mzize kisha akaamua kumweka nje kirahisi.

Nabi ambaye alimpandisha Mzize kutoka timu B kuja kikosi cha kwanza wakati akiwa naye Yanga alisema kasi ya mshambuliaji huyo, nguvu na akilia ya kukimbia kuingia kwenye eneo la hatari ndio vitu vinavyompa nafasi ya kuwa chaguo la kwanza licha ya changamoto zake zingine za ubora.

"Clement (Mzize) ni kijana mdogo lakini achana na kelele za mashabiki hakuna kocha atakayemwona au kufanya naye kazi na akaamua kutomtumia huyo ni hazina kubwa ya baadaye kwa Tanzania," alisema Nabi ambaye alizuia mshambuliaji asiuzwe Ufaransa ili Yanga ije ipate fedha nyingi baadaye.

"Mimi nilizuia asiende Ufaransa wakati ule nilitaka akomae kidogo kiubora lakini baadaye watamuuza kwa fedha nyingi zaidi, changamoto zake ni chache tu ambazo mashabiki kwa upeo wao ni vigumu kutambua Clement hajapita njia sahihi za ukuaji wake kuanzia alipokuwa mdogo.

"Changamoto hiyo inamfanya kukosa ule msingi ambao alitakiwa afundishwe akiwa mdogo namna na kuwa na utulivu wakati anakaribio uso wa lango la wapinzani Sasa hili litajengwa taratibu na atakuja kuwa sawasawa na wale waliokuwa wanamzomea watanyamaza.

"Presha hii lakini inamsaidia Mzize kama atapata washauri wazuri wanatakiwa kuendelea kumsisitiza zile kelele anatakiwa kuzigeuza faida kwake kwamba mashabiki wanataka kitu Bora zaidi au asizifuatilie kabisa awasikilize makocha wake, nilipokuwa naye nilikuwa nazungumza naye."

Wakati Nabi akiyasema hayo kocha wa Sasa wa Yanga Miguel Gamondi amewahi kuwa mbogo alipoulizwa juu ya uamuzi wa kuanza na Mzize badala ya Joseph Guede kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akisema kuna faida nyingi za kuanza na mshambuliaji huyo kinda.

"Mimi ndiye kocha ninajua kitu gani nataka kwa mchezaji kulingana na mchezo tunaocheza, Msimwangalie Mzize kwa kupoteza nafasi Kuna faida nyingi za kuwa na mchezaji kama yeye uwanjani muangalie anavyofanya wakati hatuna mpira na pia anafanya nini wakati timu inampira,"alisema Gamondi huku akiwa mkali akitetea uamuzi wake wa kuanza na mshambuliaji huyo.

Kocha Abdul Mingange alisema kupitia wasifu wa kitaaluma wa makocha wa Yanga, mchezaji huyo akiendelea kujengwa atakuwa hatari wa kucheka na nyavu na ghari sokoni.

"Ana kila kitu kinachotakiwa kwa straika, shida yake hana utulivu anapofika golini, ila anajua kukaa kwenye nafasi, anatumia nguvu kupita mbele ya mabeki, akipata mpira anaangalia golini siyo kurudisha mpira nyuma, hakuna kocha anayeweza akamuacha mchezaji kama huyo," alisema.

Kocha Said Maulidi 'SMG' aliyemfundisha kikosi cha Yanga B, alisema; "Tangu akiwa kikosi B  alikuwa ana vitu adimu  kwenye miguu yake, kasi, nguvu, kujitoa kwa timu, ni mambo machache yakumbadilisha anakosa utulivu,hilo akilifanyia kazi atafunga mabao mengi.

DATA ZAKE

Msimu huu amefunga mabao manne na asisti tano katika Ligi Kuu, wakati msimu uliopita alimaliza na mabao matano na asisti moja.

Mzize kwa sasa anahusishwa kutokana kununuliwa na Azam FC iliyoweka mezani Sh400 milioni na kama Yanga itaridhia huenda msimu ujao akiwa miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi hicho.