Sababu ya Kibu kugomea mkataba Simba hii hapa

Muktasari:

  • Ni kama yuko mlangoni kuingia kwa watani wao Yanga. Iko hivi Kibu anamaliza mkataba wake na Simba mwisho wa msimu huu lakini alipoenda mezani kuwasikiliza wekundu hao juu ya ofa yao akagundua kwamba hawajavuka hata nusu ya kiasi cha sh 400 milioni anachokihitaji achilia mbali mshahara anaoutaka.

Mwanaspoti linajua kama mambo yataenda yalivyo, wakati wowote Simba inaweza kumpoteza kiungo wao mshambuliaji mpambanaji Kibu Denis Prosper.

Ni kama yuko mlangoni kuingia kwa watani wao Yanga. Iko hivi Kibu anamaliza mkataba wake na Simba mwisho wa msimu huu lakini alipoenda mezani kuwasikiliza wekundu hao juu ya ofa yao akagundua kwamba hawajavuka hata nusu ya kiasi cha sh 400 milioni anachokihitaji achilia mbali mshahara anaoutaka.

Lakini Yanga ikawa inafuatilia mazungumzo hayo na kuamua kuingilia kati na kufika parefu anapopataka winga huyo mwenye nguvu ili akubali mkataba wao na sasa uamuzi umebaki kwake Kibu.

Yanga imefika mbali kwenye dau lake la usajili lakini pia imefika pale anapopata kuhusu mshahara wake na kilichosalia ni maamuzi tu kiungo huyo ili apande ghorofani pale kwa matajiri wa Yanga kumaliza dili lake.

Msukumo wa Yanga kumnasa Kibu umesukwa zaidi na kocha wao Miguel Gamondi ambaye amewaambia mabosi wake kuwa: “Kwanini asije kufanya kazi hapa, ana nguvu ni mtu anayejituma sana mengine tutamboresha taratibu,”amejibu Gamondi akiwaeleza mabosi wake juu ya dili hilo.

Msimu huu Kibu hana takwimu bora sana ambapo ameifungia Simba bao moja na kutoa asisti mbili kwenye mechi za ligi alizocheza mpaka sasa ingawa amekuwa akipata nafasi kubwa ya kuanza kwenye mechi za timu hiyo.

Bao pekee ambalo kibu amelifunga msimu huu ni lile la kufutia machozi wakati Yanga ikiifunga Simba kwa mabao 5-1 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi msimu huu baina ya timu hizo.

Mbali na Yanga Azam nao iko katika mawindo ya kumuwania kiungo huyo ikiwa mewasilisha ofa lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa wasimamizi wa Kibu wanapiga hesabu za mwisho za kukubali ofa ya vinara na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.

“Tunaangalia hizo ofa zote lakini mpaka sasa kama ligi ikiisha basi Kibu anaweza kwenda Yanga kwa namna mambo yalivyofika labda itokee kuna timu imerudi kwa ukubwa kuishinda ofa ya Yanga,”alidokeza mmoja wa wasimamizi wa Kibu.

KIBU NI NANI?

Alikiwasha kwenye timu kadhaa Kigoma katika ngazi za chini akaibukia Mkoani Kagera na kujiunga na Kumuyange FC iliyokuwa  Ligi Daraja la pili wakati huo ikitafuta kupanda Ligi Daraja la Kwanza lakini badae iliuzwa Dodoma na inaitwa Fountain Gate.

Ilikuwa na masikani yake mitaa ya Kumuyange na Kumunazi wilayani Ngara ilimuamini Kibu na kuwa moja ya mastaa wake mwishowe akaonekana na Geita Gold kipindi hicho ikiwa Daraja la Kwanza na kumsajili.

 Geita alicheza kwa msimu mmoja kwa kiwango bora akanunuliwa na Mbeya City ya Ligi Kuu msimu uliofuata.

Akiwa Mbeya City msimu wa 2020/2021 alicheza Ligi Kuu kwa kiwango bora na kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi hicho.

Ubora wake akiwa City ulizifanya Simba, Yanga na Azam kupigana vikumbo kutaka saini yake na mwisho wa siku Simba ikashinda na kumsaini kwa mkataba wa miaka miwili pia wakati akiwa City aliitwa kwa mara ya kwanza Taifa Stars.

Msimu wa 2021/2022, Kibu alivaa uzi wa Mnyama kwa mara ya kwanza. Usajili wa Kibu kutua Simba uliibuka suala lake la uraia kwani hakuwa na uraia rasmi wa Tanzania na asili yake ikiwa ni DR Congo. Badae akapewa uraia.

Msimu huo 2021/2022, Kibu ndiye alikuwa kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Simba kwenye ligi akiwa nayo nane na asisti nne namba ambazo washambuliaji wengine hawakuwa nazo.

Ujio wa kocha Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ulimuibua sana Kibu.

“Kibu ni mchezaji tofauti na wengi kikosini, anaweza kushambulia, anaweza kukaba ana nguvu na pumzi ya kutosha na anaweza kucheza maeneo zaidi ya matatu uwanjani,”alisemama Robertinho.