Mambo manne yaliyonogesha La Liga wikiendi

MADRID, HISPANIA. KIVUMBI cha La Liga kwa wikiendi iliyopita kilikuwa na mambo kadhaa ya kutazamwa.
Kwanza, Real Madrid ilicheza Ijumaa, wakati mahasimu wao kwenye kufukuzia ubingwa, Barcelona, yenyewe ilicheza usiku wa jana Jumatatu. Real Madrid ilishinda mechi yake na kuweka pengo la pointi 13 dhidi ya Barcelona kabla ya hawajashuka uwanjani kukipiga na Valencia usiku wa jana.
Kwenye mchakamchaka huo wa La Liga kwa mechi za wikiendi, kulikuwa na mambo manne ya kujifunza.


1. Wanaokaa benchi Real Madrid sio wanyonge
Kocha, Carlo Ancelotti alifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kilichoshinda 1-0 ugenini dhidi ya Real Sociedad, Ijumaa iliyopita. Kilichovutia kwenye mchezo huo ni kuona wachezaji ambao mara nyingi wamekuwa wakisugua benchi wakipambana na kuipa timu yao ushindi muhimu, shukrani kwa bao pekee la kipindi cha kwanza lililofungwa na Arda Guler.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 kutoka Uturuki ameshindwa kuonyesha makali na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza baada ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara tangu alipotua Hispania. Lakini, kwenye mechi hiyo alionyesha kiwango bora wakati alipotumbukiza mpira nyavuni baada ya pasi ya Dani Carvajal.

Kulikuwa na mazungumzo ya Guler kutolewa kwa mkopo msimu ujao, lakini baada ya mechi hiyo, bila ya shaka anaweza kubakizwa kwenye timu, licha ya kwamba Kylian Mbappe na Endrick wanaweza kuja kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa kiangazi na kuongeza vita kwenye ushindani wa namba.


2. Atletico yakaa pazuri kufuzu Mabingwa Ulaya
Mabao mawili ya kubabatiza yaliisaidia Atletico Madrid kuibuka na ushindi wa 3-1 nyumbani dhidi ya Athletic Bilbao na hivyo kuwafanya kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Shuti la Rodrigo de Paul lilikuwa linaelekea nje kabla ya kumbabatiza Inigo Ruiz de Galarreta na kutinga nyavuni, wakati shuti la Samuel Limo nalo lilitinga kwenye vyavu baada ya kumbabatiza kipa Unai Simon.

Hata hivyo, kilichovuruga kwenye mchezo huo ni kelele za kibaguzi za mashabiki zilizomlenga mchezaji wa Bilbao, Nico Williams huku jambo hilo likidaiwa kufanywa na kundi la mashabiki wa Atletico. Kundi hilo huko nyuma liliwahi kumfanyia ubaguzi mkubwa mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Jr na hivyo kutibua taswira ya Atletico licha ya kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

3. Girona bado kidogo michuano ya Ulaya
Girona ushindi wake wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Las Palmas uliwafanya kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa La Liga na hivyo kusubiri matokeo ya Barcelona ya usiku wa jana Jumatatu. Girona sasa imefikisha pointi 71 katika mechi 33. Matokeo ya kipigo cha Bilbao mbele ya Atletico yamekuwa na faida kubwa kwa Girona baada ya ushindi wao huo na bila ya shaka msimu ujao itaonekana kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hayo yatakuwa mafanikio makubwa, ambapo bila shaka watakuwa kwenye makubaliano na Manchester City kuona ni timu gani ya kucheza kwenye michuano hiyo ya Ulaya kutokana na timu hizo mbili zote kumilikiwa na tajiri mmoja.


4. Mambo mabaya kwa Cadiz
Cadiz sare yake ya 1-1 nyumbani kwenye mchezo dhidi ya Mallorca, juzi Jumapili ilikuwa mbaya kwao kwa sababu kukosa ushindi kumewafanya kushindwa kutoka kwenye timu tatu za mkiani kwenye msimamo wa La Liga.

Ushindi kwenye mechi hiyo ungewafanya Cadiz kuongeza pointi tatu ambazo zingewatoa kwenye hatari hiyo ya kushuka daraja, lakini sare sasa wamejikuta wakiwa nyuma kwa pointi sita dhidi ya Mallorca na tano dhidi ya Celta, ambao walichapwa na Alaves, Jumamosi.

Cadiz tatizo lao si kupata pointi tano katika mechi tano zilizobaki, bali ni mchezo wao ujao, wana kibarua cha kukabilisna na Real Madrid, ambayo bila ya shaka itakuwa na kazi ya kufanya ili kubeba ubingwa msimu huu