Eti kama vipi apewe Tuchel

MANCHESTER, ENGLAND. KIPA mkongwe, Peter Schmeichel anaamini Thomas Tuchel atakuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi cha Manchester United kama atanyakuliwa kwenda kurithi mikoba ya Erik ten Hag huko Old Trafford.

Ten Hag yupo kwenye presha kubwa kwenye ajira yake huko Old Trafford baada ya msimu wa pili mgumu kwake.
Kikosi hicho kwa sasa kinapambana na hali yake huku kikiwa hakina uwezo wowote wa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na kuweka rekodi ya kumaliza nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi msimu huu.

Tajiri mpya wa Man United, Sir Jim Ratcliffe bado hajafanya uamuzi wa kuhusu kocha huyo, amfukuze au abaki naye, lakini matokeo ya mechi zilizobaki yatakuwa na athari kubwa kwenye hatima ya kocha huyo.

Tuchel ni mmoja kati ya makocha wengi wanaohusishwa na Man United baada ya Mjerumani huyo kuripotiwa ataachana na Bayern Munich itakapofika mwisho wa msimu huu.
Schmeichel, ambaye ni gwiji wa Old Trafford, anaamini kocha huyo wa zamani wa Chelsea atakuwa na faida kubwa atakapotua Man United kama ambavyo Jurgen Klopp alifanya alipotua Liverpool miaka tisa iliyopita.
Schmeichel alisema: “Nampenda. Nampenda
Thomas Tuchel. Nilipata bahati ya kumhoji mara kadhaa. Uelewa wake wa soka ni mkubwa sana. Nadhani amekuwa na bahati mbaya tu kwa kuwa kwenye klabu mbili kubwa kwenye nyakati mbaya kihistoria na hivyo kushindwa kuonyesha makali yake.
“Si kwamba alifanya vibaya Chelsea. Alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya pale, sivyo?
Amekuwa na mipango mingi mizuri. Si vyema kulinganisha watu, lakini naamini atakachokuja kuleta Man United kitafanana na kile alichofanya Klopp alipotua Liverpool.”

Tajiri Ratcliffe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa kuhusu kocha kwenye kikosi hicho, huku Ten Hag akitazamwa kwa mechi zilizobaki na kuona kama atashinda ubingwa wa Kombe la FA kwa kuwafunga Manchester City, Wembley.