Jamie Vardy aipa ubingwa Leicester City akifikisha mabao 190

Leicester, England. Staa wa Leicester City, Jamie Vardy juzi alifunga mabao mawili na kuipa timu yake ubingwa wa Championship wakiwa tayari wameshapanda daraja.

Leicester ilifanikiwa kuichapa Preston North End mabao 3-0 na kuchukua ubingwa huo ikiwa ni msimu mmoja tu tangu timu hiyo iliposhuka daraja kutoka Ligi Kuu England.

Vardy mwenye miaka  37, ambaye mabao yake huko nyuma yaliwahi kuipa Leicester ubingwa wa Ligi Kuu England na Kombe la FA, amefikisha mabao 20 kwenye michuano yote  msimu huu.

Kasey McAteer, naye alifanikiwa kufunga bao moja na kuifanya timu hiyo ipande ikiwa sawa na  Burnley, Fulham na Norwich ambazo zilikaa chini msimu mmoja tu na kupanda, zikiwa zimetwaa ubingwa.

Ushindi huo pia umeifanya Leicester kuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Championship mara mbili, lakini kama itashinda mechi ya mwisho itafikisha pointi 100 na kuweka rekodi nyingine ya kukusanya pointi nyingi kwa msimu.

Kocha wa Leicester  Enzo Maresca, ambaye alipewa kikosi hicho baada ya kushuka, amesema kitendo cha timu hiyo kushuka na kupanda haraka, kinaonyesha kuwa ni timu bora na yenye wachezaji wanaoweza kujituma.

"Hatimaye tumefanikiwa kupanda daraja na kutwaa ubingwa huu, nafikiri tumeipeleka timu hii sehemu ambayo ilikuwa inastahili kuwa.

“Kwenye matukio kama haya, furaha ni jambo la msingi sana, lakini nataka kuwaeleza mashabiki kuwa huu ni muda wa kufurahi.

“Tunatakiwa kuwashukuru wachezaji wetu wote kwa kiwango walichoonyesha kwenye michezo yetu yote ya msimu huu,” alisema kocha huyo ambaye ameiongoza timu hiyo kufunga mabao 89 kwenye michezo 45.


Kwenye kipindi cha miaka 12 ambayo Vardy amekaa na Leicester amefanikiwa kufunga mabao 190, kwenye michezo 463.

Timu nyingine za Leeds United na Ipswich Town zinapambana kurejea kwenye ligi msimu ujao, kila moja ikiwa na pointi tisini, zikiwa zimebakiza mechi moja msimu umalizike.