Kane amganda Lewandowski

MUNICH, UJERUMANI. MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Harry Kane, ambaye alifunga mabao yote mawili katika ushindi wao wa mabao 2-1 wikiendi iliyopita nyumbani dhidi ya Eintracht Frankfurt, amesema “inawezekana” ataivunja rekodi ya Bundesliga ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja.

Akicheza msimu wake wa kwanza nchini Ujerumani, Kane amefunga mabao 35 katika mechi 31 za ligi  -- mabao sita pungufu ya aliyofunga Robert Lewandowski anayeshikilia rekodi ya muda wote kwa kufunga mabao 41 msimu wa 2020/21.

“Inawezekana, lakini napaswa kukomaa sana,“ alisema Kane ambaye amebakisha mechi tatu msimu kuisha.

“Nahitajika kufunga mabao kadhaa wiki ijayo. Rekodi iko pale inafikika.

“Itategemea na mechi chache zijazo. Lakini ilikuwa jambo zuri kufunga (wikiendi) na kuisaidia timu kupata ushindi.”

Mabao hayo mawili ya Kane dhidi ya Frankfurt yalimaanisha kwamba amezifunga timu 16 kati ya wapinzani wao 17 wa Bundesliga msimu huu, akishindwa kuifunga Freiburg tu.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 30 sasa ana mabao 42 katika michuano yote msimu huu, idadi ambayo ni rekodi binafsi katika maisha yake ya soka kufunga ndani ya msimu mmoja.

Leo Jumanne, Kane anatarajiwa kuwa uwanjani nyumbani Allianz Arena kuikabili Real Madrid katika mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Natumaini nitaingia na hali hii ya kujiamini katika mechi ya Jumanne,” aliongeza.
“Itakuwa mechi ngumu sana, tutapaswa kucheza kwa kiwango cha juu kama tulivyocheza dhidi ya Arsenal (katika robo fainali)  -- na tuboreshe zaidi.

“Real ni timu kubwa, klabu yao ina historia bora katika michuano hii.”

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Kane kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Alikosa nusu fainali zilizopita kutokana na majeraha lakini akarejea kucheza fainali ya msimu wa 2018-19, ambayo Tottenham ilipasuka 2-0 dhidi ya Liverpool.

WASIOFUNGIKA
Licha ya ushindi ambao uliifanya Bayern kufikisha pointi 69 katika nafasi ya pili ya msimamo wa Bundesliga, bado haijajihakikishia kumaliza katika nafasi hiyo kwani imeipita VfB Stuttgart iliyo katika nafasi ya tatu kwa pointi tano na imeizidi RB Leipzig kwa pointi 7 huku zikibaki mechi tatu.

Stuttgart yenye pointi (64), Leipzig (62) na Borussia Dortmund iliyo na pointi 57 katika nafasi ya tano, ndizo timu pekee zinazoendelea kupigania kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa sababu Eintracht Frankfurt iliyo katika nafasi ya sita ina pointi 45 hivyo hata ikishinda mechi zake tatu zilizobaki haiwezi kuifikia Dortmund.

SV Darmstadt yenye pointi 17 imeshuka daraja baada ya wikiendi iliyopita kufungwa 1-0 nyumbani na Heidenheim, wakati FC Cologne iliyo katika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 23 inaweza kujiokoa.
Kuanzia timu iliyo katika nafasi ya 13 ya Borussia Monchengladbach yenye pointi 32, Union Berlin (30), VfL Bochum (30) na Mainz (28) zote zimekalia kuti kavu.

Mabingwa Bayer Leverkusen wameboresha rekodi yao ya kutopoteza mchezo hata mmoja msimu huu kufikia mechi 46 za michuano yote ikijiokoa kwa bao la dakika ya mwisho katika sare ya 2-2 dhidi ya VfB Stuttghart wikiendi iliyopita.