Kane Kiatu cha Ulaya kinamhusu

MUNICH, UJERUMANI. STRAIKA, Harry Kane msako wa taji lake la kwanza kwenye klabu mpya huko Bayern Munich huenda ukaendelea hadi msimu ujao, lakini staa huyo wa England anaweza kujifariji kwa kubeba tuzo binafsi na kuweka kabatini kwake.

Kane, 30, amekuwa moto kwa kupasia nyavu tangu alipojiunga na Bayern Munich akitokea Tottenham Hotspur wakati wa uhamisho wa dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana kwa ada ya Pauni 100 milioni.

Mabao yake mawili aliyofunga kwenye ushindi wa 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt, Jumamosi iliyopita umemfanya afikishe mabao 35 kwenye Bundesliga msimu huu.

Sasa anaongoza kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, akiwa na mabao tisa zaidi ya mchezaji anayemfuatia, Kylian Mbappe, aliyefunga mara 26 kwenye ligi akiwa na kikosi cha Paris Saint-Germain msimu huu.

Staa wa Stuttgart, Serhou Giurassy yupo kwenye nafasi ya tatu na mabao yake 25, lakini kinachoonekana si yeye wala Mbappe mwenye uwezo wa kumfikia Kane.

Sasa Kane yupo kwenye nafasi nzuri ya kuingia kwenye anga za masupastaa Lionel Messi na Crisitiano Ronaldo waliowahi kushinda tuzo hiyo na wakali hao wameshinda Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya mara 10.

Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya kinatolewa kwa mchezaji aliyefunga mabao mengi kwenye ligi za ndani kuliko wengine, huku kila bao likihesabiwa kwa pointi na mwenye ambaye amekusanya pointi nyingi, ndiye mshindi.

Messi alishinda tuzo hiyo mara sita wakati anakipiga Barcelona, wakati Ronaldo alishinda tuzo nne, moja akiwa Manchester United na tatu alipojiunga na Real Madrid.